Reuters: RSF imetia saini hati ya kuunda serikali nyingine nchini Sudan
Wanasiasa wa Sudan, Al-Hadi Idris na Ibrahim Al-Mirghani, wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) limetia saini mkataba na makundi washirika ya kisiasa na yenye silaha wa kuunda "serikali ya amani na umoja" sambamba na ile ya sasa nchini humo katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo.
Idris, afisa wa zamani na mkuu wa Sudanese Revolutionary Front, amesema kuundwa kwa serikali hiyo kutatangazwa kutoka ndani ya nchi katika siku zijazo.
Idris na Al-Mirghani wametia saini mkataba huo, pamoja na kiongozi wa Sudan People's Liberation Movement-North, Abdelaziz Adam al-Hilu, ambaye majeshi yake yanadhibiti maeneo makubwa ya ardhi katika Jimbo la Kordofan Kusini.
Hata hivyo wachambuzi wa siasa wanasema serikali ya aina hiyo, ambayo tayari imezua wasiwasi katika Umoja wa Mataifa, haitatambuliwa kimataifa.
Kwa mujibu wa hati ya mkataba huo, waliotia saini wamekubaliana kuwa Sudan inapaswa kuwa "nchi isiyo na misingi ya dini, ya kidemokrasia na yenye tawala za majimbo" na jeshi moja la kitaifa, lakini ikihifadhi haki ya makundi yenye silaha kuendelea kuwepo.
Kenya ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo yaliyoanza wiki jana na kuzua shutuma kutoka Sudan na ukosoaji wa ndani nchini Kenya dhidi ya Rais William Ruto kwa kuiingiza nchi hiyo katika mzozo wa kidiplomasia na nchi nyingine.
Kama hatua ya kupinga kitendo hicho cha Kenya, serikali ya Sudan imuondoa balozi wake mjini Nairobi, licha ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya kusisitiza kwamba itaendelea kushikamana na sera ya kutopendelea upande wowote katika mgogoro wa Sudan.