Senegal yasaini makubaliano ya amani na kundi linalopigania kujitenga eneo la Casamance
Serikali ya Senegal na harakati kwa jina la Movement of Democratic Forces of Casamance (MFDC); kundi la waasi linalopigania kujitenga eneo la kusini mwa Senegal la Casamance wametia saini makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo, na hivyo kumaliza moja ya migogoro mikongwe zaidi barani Afrika, ambayo imedumu kwa miongo minne.
Shirika la habari la Senegal limemnuku Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ousmane Sonko baada ya kuzungumza na waandishi wa habari katika ikulu ya Rais wa Guine Bissamu kwamba: Wameweza kushiriki katika kukamilisha makubaliano haya muhimu, ambayo yanajumuisha hatua kubwa sana kuelekea amani ya uhakika katika eneo la Casamance kusini mwa Senegal.
Eneo la Casamance ambalo lilitenganishwa na eneo la kaskazini mwa Senegal na Gambia, ni eneo lililodumu na mvutano wa muda mrefu zaidi barani Afrika, ulioanza mwaka 1982 na kusababisha kuuawa maelfu ya watu na kuathiri vibaya uchumi wa eneo hilo.
Kundi la waasi wa MFDC ambalo limeendesha mapambano kwa muda mrefu kwa ajili ya kujitenga eneo la Casamance huko kusini mwa Senegal katika mpaka na nchi jirani ya Gambia liliasisiwa mwaka 1982. Mwezi Mei mwaka juzi, wapiganaji wa kundi hilo wasiopungua 250 walisalimisha silaha zao katika ngome yao kuu za zamani huko Mongone.