Viongozi wa Libya na Somalia wajadiliana ushirikiano katika uwekezaji na elimu
Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya, Mohamed Menfi, amesisitizia umuhimu wa kuweko ushirikiano baina ya nchi yake na Somalia katika nyuga tofauti. Mwito huo aliutoa jana Jumatatu katika mazungumzo ya pamoja na waandishi wa habari baina yake na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia aliyeko ziarani nchini Libya.
Kwa mujibu wa Menfi, nchi hizo mbili zimetiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano inayohusu uwekezaji, mafunzo na elimu.
Katika sehemu moja ya matamshi yake, Menfi amesema: "Tunatilia mkazo uungaji mkono wetu kwa Somalia kama ambavyo pia tuna imani Somalia nayo itaendelea kutekeleza jukumu lake muhimu kwenye majukwaa na mashirika ya kimataifa katika kipindi hiki cha ushirikiano mzuri baina yetu."
Vilevile amegusia fursa za uratibu wa pamoja zilizopo baina ya nchi hizo mbili kutokana na kwamba zote mbili ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, hivi sasa Somalia ina fursa nzuri kutokana na kuwa kwake mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa anayewakilisha Afrika akishirikiana na Algeria na Sierra Leone.
Menfi ameonesha pia matumaini yake ya kupata uungaji mkono wa Somalia katika jitihada zake za kusimamisha uadilifu na utulivu na juhudi za kuitisha uchaguzi wa bunge na urais huko Libya.
Kwa upande wake, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia ametilia mkazo umuhimu wa kuendelezwa uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili, na kuahidi kuwa Somalia itaendelea kuiunga mkono Libya.
Mapema jana Jumatatu, Waziri Mkuu wa Libya, Abdul Hamid Dbeibah alikutana na Rais Mohamud na kujadiliana uhusiano wa pande mbili na masuala ya kikanda.