Sudan yatishia kulipiza kisasi dhidi ya Kenya kwa kuwa mwenyeji wa RSF
Serikali ya Sudan jana Jumatatu iliapa kuchukua hatua kali dhidi ya Kenya kutokana na Nairobi kuwa mwenyeji wa kikao cha wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan, Hussein al-Amin amesema katika mazungumzo na waandishi wa habari huko Port Sudan kwamba: "Tutawasilisha barua yetu kwa Umoja wa Afrika na mashirika mengine ya kimataifa na tutachukua hatua za kulipiza kisasi dhidi ya Kenya kutokana na misimamo yake ya kiuadui dhidi ya Sudan."
Amesema: "Tutachukua hatua za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kuingia bidhaa za Kenya nchini mwetu hasa kwa vile Sudan ni moja ya masoko makubwa ya chai ya Kenya."
Afisa huyo wa Sudan ameishutumu Kenya kuwa inawaunga mkono wanamgambo wa RSF ambao wamekuwa wakipigana na Jeshi wa Sudan (SAF) tangu katikati ya mwezi Aprili 2023.
Aidha ameiita hatua ya Kenya kuwa mwenyeji wa sherehe za kutiwa saini makubaliano baina ya RSF na washirika wake ya kuundwa serikali nyingine nchini Sudan kuwa ni "kitendo cha uadui na ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya Sudan."
Amesema: Hatua hiyo ya Kenya ni ukiukaji wa mikataba na makubaliano yote ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali na mengineyo.
Siku chache zilizopita, makundi ya upinzani ya Sudan, ikiwa ni pamoja na RSF, yametia saini mkataba wa kuanzisha serikali nyingine ya kiraia nchini Sudan sambamba na ile inayoongozwa na jeshi la nchi hiyo SAF.