DRC Yasitisha Usafirishaji wa Kobalti kwa Miezi Minne
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123210-drc_yasitisha_usafirishaji_wa_kobalti_kwa_miezi_minne
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesitisha usafirishaji wa kobalti kwa miezi minne ili kudhibiti usambazaji wa kobalti kwenye soko la kimataifa, ambalo kwa sasa linakabiliwa na upitilivu wa bidhaa hiyo. Hali hii imesababisha kushuka kwa bei kwa mfululizo.
(last modified 2025-02-25T22:51:49+00:00 )
Feb 25, 2025 22:51 UTC
  • DRC Yasitisha Usafirishaji wa Kobalti kwa Miezi Minne

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesitisha usafirishaji wa kobalti kwa miezi minne ili kudhibiti usambazaji wa kobalti kwenye soko la kimataifa, ambalo kwa sasa linakabiliwa na upitilivu wa bidhaa hiyo. Hali hii imesababisha kushuka kwa bei kwa mfululizo.

Uamuzi huu unalenga "kuimarisha ufuatiliaji na udhibiti wa mnyororo wa usambazaji na kukuza uchakataji wa madini hayo ndani ya nchi," Wizara ya Madini ya DRC ilisema, ikinukuu taarifa ya mdhibiti wa madini wa Kongo kama ufafanuzi wake.

Shirika hilo lilisema kuwa uamuzi wa kusitisha usafirishaji wa kobalti unaweza kufanyiwa mapitio ndani ya miezi mitatu.

Kusitishwa huku kunakuja wakati mgogoro unaendelea mashariki mwa DRC. Tangu Januari, mapigano yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 7,000, wengi wao wakiwa raia. Hayo yametangazwa naWaziri Mkuu Judith Suminwa Tuluka mjini Geneva siku ya Jumatatu.

Hayo yamejiri wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC zimewateua Uhuru Kenyatta kutoka Kenya, Olusegun Obasanjo kutoka Nigeria, na Hailemariam Desalegn kutoka Ethiopia kuongoza mazungumzo ya kutatua mzozo wa mashariki mwa DRC, eneo lenye utajiri wa madini yakiwemo kobalti.