Somalia na Umoja wa Afrika wakubaliana kuhusu wanajeshi watakaojumuishwa katika kikosi kipya
Serikali kuu ya Somalia na Umoja wa Afrika wamekubaliana kuhusu idadi ya wanajeshi kutoka nchi mbalimbali watakaohudumu katika kikosi kipya cha Umoja wa Afrika.
Maafikiano hayo yamefikiwa kufuatia wiki kadhaa za mtafaruku kati ya Ethiopia na Somalia na pia kati ya Somalia na Burundi.
Afisa wa Umoja wa Afrika ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameziuambia duru za habari kwamba, wanajeshi wa Burundi ambao wamekuwa nchini Somalia tangu 2007 wataondoka nchi humo baada ya serikali za nchi hizo mbili kushindwa kukubaliana kuhusu idadi ya wanajeshi kutoka Burundi.
Kulingana na maafisa wa Somalia na Umoja wa Afrika ni kuwa, kikosi kipya cha Umoja wa Afrika cha kusaidia katika juhudi za kurejesha amani nchini Somalia, AUSSOM, kinatarajiwa kuwa na wanajeshi 11,900 ardhini nchini Somalia, wakiwemo wanajeshi, polisi na wafanyakazi raia.
Mkataba huo mpya unasema kutakuwa na wanajeshi 4,500 kutoka Uganda, 2,500 kutoka Ethiopia, 1,520 kutoka Djibouti, 1,410 kutoka Kenya na 1,091 kutoka Misri, kulingana na maafisa hao.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.