Ugonjwa usiojulikana waua makumi nchini DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123268-ugonjwa_usiojulikana_waua_makumi_nchini_drc
Watu wasiopungua 53 wamefariki kutokana na ugonjwa usiojulikana katika wiki za hivi karibuni katika sehemu ya kaskazini-magharibi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2025-02-27T04:24:06+00:00 )
Feb 27, 2025 04:24 UTC
  • Ugonjwa usiojulikana waua makumi nchini DRC

Watu wasiopungua 53 wamefariki kutokana na ugonjwa usiojulikana katika wiki za hivi karibuni katika sehemu ya kaskazini-magharibi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo  limesema kuwa visa 431 vimeripotiwa katika milipuko miwili kwenye maeneo ya mbali ya jimbo la Équateur kufikia Februari 15. Katika kijiji cha Bomate, watu 45 wamefariki kati ya visa 419 vilivyojulikana. WHO imesema vifo jumla ya vinane kati ya visa 12 viliripotiwa awali katika vijiji vya karibu vya Boloko na Danda.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa, baridi, maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili, kutokwa na jasho, ugumu wa shingo, kikohozi, kutapika, kuhara, na maumivu ya tumbo. Kwa mujibu wa WHO karibu nusu ya vifo vinadaiwa kutokea ndani ya saa 48 baada ya dalili za kwanza kuonekana.

Msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic amesema: "Milipuko hii, ambayo imeona ongezeko la haraka la visa ndani ya siku chache, inahatarisha afya ya umma kwa kiwango kikubwa. Sababu halisi bado haijajulikana."

Katika taarifa yake ya hivi karibuni, shirika hilo la afya duniani lilisema kuwa sampuli kutoka kwa wagonjwa 12 waliokuwa hai na mgonjwa mmoja aliyefariki zilipimwa na hazikupatikana na Ebola au Marburg. Timu za afya zinaendelea kuchunguza sababu nyingine zinazoweza kuwa chanzo, ikiwa ni pamoja na malaria, homa ya virusi inayosababisha kutokwa na damu, sumu ya chakula au maji, homa ya matumbo, na ugonjwa wa uti wa mgongo.

Ugonjwa huu wa hivi punde, ambao unaripotiwa kuanza katika kijiji cha Boloko baada ya watoto watatu kula popo aliyekufa na kufariki ndani ya saa 48, unajiri wakati nchi hiyo ya Afrika ya Kati ikikabiliana na changamoto nyingine za kiafya pamoja na vita katika eneo la mashariki.