Wasomali 4.4 wanaweza kukabiliwa na njaa kufikia Aprili 2025
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123272-wasomali_4.4_wanaweza_kukabiliwa_na_njaa_kufikia_aprili_2025
Serikali ya Somalia na mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yalionya Jumatano kuwa watu milioni 4.4 wanaweza kukabiliwa na njaa kufikia Aprili 2025 kutokana na ukame unaozidi, mizozo na ongezeko la bei za chakula katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 
(last modified 2025-02-27T04:31:21+00:00 )
Feb 27, 2025 04:31 UTC
  • Wasomali 4.4 wanaweza kukabiliwa na njaa kufikia Aprili 2025

Serikali ya Somalia na mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yalionya Jumatano kuwa watu milioni 4.4 wanaweza kukabiliwa na njaa kufikia Aprili 2025 kutokana na ukame unaozidi, mizozo na ongezeko la bei za chakula katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 

Kamishna wa Wakala wa Usimamizi wa Maafa ya Somalia Mohamuud Moallim, amesema katika taarifa ya pamoja na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa kuwa: "Ukame unaozidi kuwa mbaya unaleta tishio kubwa kwa jamii ambazo tayari zinakabiliana na shida kubwa na mizozo endelevu. " Amebaini kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kuokoa maisha, kulinda riziki, na kuzuia mateso zaidi.

Afisa huyo wa Somalia  ameongeza kuwa wakati huu, hawakabiliani tu  na athari mbaya za ukame bali pia kuna hatari zingine zinazochangia, ikiwa ni pamoja na mizozo na upungufu wa fedha za misaada ya kibinadam. 

Onyo hilo lilitolewa na Wakala wa Usimamizi wa Maafa ya Somalia pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu (OCHA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF), na Mpango wa Chakula wa Ulimwenguni wa Umoja wa Mataifa (WFP)

Mashirika hayo ya misaada yanahofu kuwa idadi ya watu wanaoweza kuathirika itaongezeka hadi milioni 4.4 (yaani asilimia 23 ya idadi ya watu) kati ya Aprili na Juni 2025, wakati ambapo mvua chini ya wastani inatarajiwa. 

Taarifa hiyo imesema kuwa upungufu mkubwa wa fedha umepelekea kupunguzwa au kukatwa kwa programu za kuokoa maisha nchini Somalia, na kuwa dharura kuongeza misaada ya chakula, usaidizi wa lishe, huduma za maji na usafi wa mazingira, na mipango ya kuimarisha riziki ili kupunguza athari za ukame unaotarajiwa nchini Somalia

Mpango wa Mahitaji na Majibu ya Kibinadamu wa Somalia kwa mwaka 2025 unahitaji dola bilioni 1.42 ili kukabiliana na hali hiyo ya mgogoro, lakini kwa sasa ni asilimia 12.4 tu ya kiasi hicho ndiocho kimepatikana 

Onyo hilo linakuja wakati uchunguzi wa hivi karibuni wa taasisi ya Usalama wa Chakula (IPC) unaonyesha kuwa Wanasomali milioni 3.4 tayari wanakabiliwa na hali ya njaa ya kiwango cha mgogoro au zaidi

Nchi hiyo iko karibu na hali ya njaa kama ile ya mwaka 2022, ambayo kulingana na data za Umoja wa Mataifa, iliua maelfu ya watu, karibu nusu yao wakiwa watoto.