Rais Ramaphosa: Mivutano ya kisiasa inakwamisha maendeleo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123300-rais_ramaphosa_mivutano_ya_kisiasa_inakwamisha_maendeleo
Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa, mivutano ya kisiasa inatishia maendeleo ya dunia na kwamba ulimwengu utaendelea kurudi nyuma kutokana na kukosekana uthabiti na ushirikiano wa kimataifa.
(last modified 2025-02-27T23:13:57+00:00 )
Feb 27, 2025 23:13 UTC
  • Rais Ramaphosa: Mivutano ya kisiasa inakwamisha maendeleo

Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa, mivutano ya kisiasa inatishia maendeleo ya dunia na kwamba ulimwengu utaendelea kurudi nyuma kutokana na kukosekana uthabiti na ushirikiano wa kimataifa.

Ramaphosa amesema hayo katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa mkutano huo mawaziri wa fedha wa G20 unaowakusanya mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu kutoka mataifa hayo 20 yanayoongoza kiuchumi ulimwenguni.

Rais wa Afrika Kusini alionya dhidi ya kile alichokiita mmomonyoko kwenye mahusiano ya kimataifa.

"Kwenye wakati huu wa mitikisiko ya siasa za kilimwengu, utaratibu uliojikita kwenye sheria una umuhimu mkubwa hasa katika kutumika kama chombo cha kutatua mizozo na migogoro." Alisema rais huyo wa Afrika Kusini.

Ramaphosa aliuambia mkutano huo uliofanyika mjini Cape Town kwamba, ushirikiano wa kimataifa ndio tumaini pekee kwenye kuzikabili changamoto zisizotarajiwa, zikiwemo za kasi ndogo ya ukuwaji wa uchumi, kupanda kwa mzigo wa madeni, ufukara na ukosefu wa usawa unaozidi kukua, na kitisho cha kutokomea sayari ya dunia kinachosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Katika mkutano huo, Waziri wa Fedha wa Italia, Giancarlo Giorgetti, aliunga mkono wito wa Rais Ramaphosa, akisema kuwa mitafaruku kwenye siasa za kilimwengu inatishia kuusambaratisha uchumi wa dunia, hasa kwenye mataifa masikini zaidi.

 "Dhana ya kujilinda kiuchumi, viunzi vya biashara na ukosefu wa uhakika kwenye siasa ni mambo yanayotishia ukuwaji wa uchumi na mnyororo wa thamani ulimwenguni, yanaongeza gharama za uzalishaji na bei za bidhaa muhimu na yanadhoofisha uhimilivu wa kiuchumi." Aliongeza Giogretti.