ICC yaunga mkono kuundwa mahakama maalum kuchunguza uhalifu DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123302-icc_yaunga_mkono_kuundwa_mahakama_maalum_kuchunguza_uhalifu_drc
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetangaza kuunga mkono kuundwa mahakama maalumu ya kuchunguza uhalifu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
(last modified 2025-02-27T23:14:21+00:00 )
Feb 27, 2025 23:14 UTC
  • ICC yaunga mkono kuundwa mahakama maalum kuchunguza uhalifu DRC

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetangaza kuunga mkono kuundwa mahakama maalumu ya kuchunguza uhalifu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) amesema kuwa, mahakama za kimataifa zimeshindwa kukomesha ukatili wa miongo mitatu katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Eneo la mashariki mwa DRC, ambalo limekumbwa na miongo kadhaa ya mzozo usiokoma, limetumbukia katika machafuko mapya baada ya waasi wa M23 kuteka maeneo makubwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Katika mahojiano na shirika la habari la AFP wakati wa ziara yake mjini Kinshasa, mwendesha mashtaka wa ICC Karim Khan alikiri kushindwa kwa mfumo wa mahakama za kimataifa kukomesha ukatili wa kutisha ulioambatana na miongo kadhaa ya migogoro katika eneo hilo. Alisema “ana wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa machafuko”.

ICC ambayo iliwatia hatiani watu watatu kwa makosa ya ukatili mashariki mwa DRC, hivi sasa inachunguza uhalifu zaidi katika eneo hilo, “ikiangazia hadithi mbaya kutoka mashariki mwa Congo”, alisema.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ameunga mkono pendekezo la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo la kuundwa mahakama maalum kwa ajili ya nchi hiyo, ambayo inatarajiwa kujadiliwa mwezi Aprili katika mkutano wa kimataifa mjini Kinshasa.