UN yawashutumu viongozi wa Sudan Kusini kwa kuchochea ghasia, machafuko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123368-un_yawashutumu_viongozi_wa_sudan_kusini_kwa_kuchochea_ghasia_machafuko
Umoja wa Mataifa umesema viongozi wa Sudan Kusini wanaendelea kuchochea ghasia na ukosefu wa amani nchini humo, huku mivutano ya kuwania madaraka, ufisadi na migawanyiko ya kikabila ikiendelea.
(last modified 2025-03-01T09:01:53+00:00 )
Mar 01, 2025 09:01 UTC
  • UN yawashutumu viongozi wa Sudan Kusini kwa kuchochea ghasia, machafuko

Umoja wa Mataifa umesema viongozi wa Sudan Kusini wanaendelea kuchochea ghasia na ukosefu wa amani nchini humo, huku mivutano ya kuwania madaraka, ufisadi na migawanyiko ya kikabila ikiendelea.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema viongozi wa Sudan Kusini wanaendelea kuchochea ghasia na ukosefu wa utulivu katika nchi hiyo changa zaidi duniani, ambayo ilijipatia uhuru mwaka 2011.

Ripoti hiyo imesema, nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta, inasumbuliwa na umaskini, vita vya kuwania madaraka, ufisadi na migawanyiko ya kikabila, ambayo inazuia harakati za kurejeshwa utulivu na maendeleo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ambayo imetokana na uchunguzi uliofanywa mwaka 2024, nyaraka hizo zinaonyesha kuwa viongozi wa kisiasa na kijeshi nchini Sudan Kusini wanaendelea kuchochea migogoro na ghasia.

Ripoti hiyo imetayarishwa kupitia mikutano na maafisa wa serikali za mitaa, uchambuzi wa hati, na habari za kiuchunguzi ambazo zinathibitisha kuendelea migogoro na mauaji ya kiholela, pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu kama vile unyanyasaji wa kingono, kutumia watoto kwa nguvu kama wanajeshi, utekaji nyara kwa ajili ya utumwa wa ngono.

Mapema mwezi huu, mapigano yalizuka katika maeneo mawili ya Sudan Kusini na kuua raia na kumjeruhi mwanajeshi mmoja wa kulinda amani. Mapigano hayo pia yamewalazimisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linahofia kwamba mzozo huo huenda ukaongezeka katika siku zijazo.