Kipindupindu chaua zaidi ya watu 200 nchini Angola
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123376-kipindupindu_chaua_zaidi_ya_watu_200_nchini_angola
Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mripuko wa hivi karibuni wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Angola imeongezeka na kupindukia 200.
(last modified 2025-03-01T23:00:46+00:00 )
Mar 01, 2025 23:00 UTC
  • Kipindupindu chaua zaidi ya watu 200 nchini Angola

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mripuko wa hivi karibuni wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Angola imeongezeka na kupindukia 200.

Katika taarifa yake ya jana, Wizara ya Afya ya Angola imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, watu 5,574 wameambukizwa ugonjwa huo tangu mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu na 201 kati yao wameshafariki dunia. 

Kesi za kipindupindu zimeripotiwa katika majimbo 13 kati ya 21 ya Angola. Mripuko huo ulianzia katika jimbo kuu la Luanda, ambalo limerekodi idadi kubwa ya wagonjwa, likifuatiwa na majimbo jirani ya Bengo na Icolo e Bengo.

Katikati ya mwezi uliopita wa Februari, Wizara ya Afya ya Angola ilitangaza kuwa, karibu watu 108 wamefariki dunia nchini humo kutokana na mripuko wa kipindupindu tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Takwimu hizo zilitolewa huku idadi ya vifo nayo ikiripotiwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Angola, karibu nusu ya maambukizi ya kipindupindu yameripotiwa katika mji mkuu Luanda. Wizara hiyo ilisema kuwa,  walioambukizwa ni watu wenye umri wa kuanzia miaka miwili.

Hadi katikati ya Februari, watu waliofariki duniani kwa ugonjwa huo mkoani Luanda walikuwa ni 48. Idadi hiyo imeongezeka sana katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja uliopita.

Wizara ya Afya ya Angola imesema kuwa kuna changamoto nyingi inazokabiliana nazo katika kudhibiti mripuko huo, hususan usafi wa mazingira katika maeneo yaliyoathirika zaidi na ukosefu wa mifumo ya maji safi ya kunywa katika maeneo hatarishi.