Ramadhani imeanza na mgogoro wa vita unaendelea nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123382-ramadhani_imeanza_na_mgogoro_wa_vita_unaendelea_nchini_sudan
Sambamba na kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jeshi la Sudan SAF limezidisha mashambulizi ya kuuteka kikamilifu mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, kutoka mikononi mwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF). Hata hivyo kampeni hiyo inasababisha hasara kubwa hasa kwa watoto wa nchi hiyo. Mapigano hayo yamesambaratisha maisha ya vijana na kushadidisha njaa, mbali na janga la majeruhi, wajane na mayatima.
(last modified 2025-03-01T23:02:46+00:00 )
Mar 01, 2025 23:02 UTC
  • Ramadhani imeanza na mgogoro wa vita unaendelea nchini Sudan

Sambamba na kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jeshi la Sudan SAF limezidisha mashambulizi ya kuuteka kikamilifu mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, kutoka mikononi mwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF). Hata hivyo kampeni hiyo inasababisha hasara kubwa hasa kwa watoto wa nchi hiyo. Mapigano hayo yamesambaratisha maisha ya vijana na kushadidisha njaa, mbali na janga la majeruhi, wajane na mayatima.

Mtandao wa Africanews umeandika makala maalumu kuhusu hali mbaya ya Sudan na sehemu moja ya makala hiyo imesema: "Katika hospitali ya Omdurman, tukio la kusikitisha sana linaziumiza nyoyo; msichana mdogo anapiga mayowe ya uchungu na maumivu kutokana na majeraha ya moto yaliyosababishwa na mripuko. Mama yake, Khadija, pia ameungua vibaya baada ya kujitolea muhanga maisha yake katika jitihada za kumwokoa mwanawe huyo. Familia hiyo ilinusurika na kifo katika shambulio la makombora, lakini imepoteza kila kitu huku mama mtoto akihangaika kumudu angalau mahitaji ya kimsingi lakini hana uwezo hata wa kulipia pesa za bandeji za bintiye.

Limeandika: Hospitali hiyo imejaa wagonjwa watoto, wengi wao wakiuguza majeraha yanayotokana na vita, utapiamlo na magonjwa. Kwa mujibu wa Dk. Maha Hussein, Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya Omdurman, vita vinavyoendelea baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF vimezusha wimbi la idadi kubwa ya watoto wanaohitaji matibabu ya haraka.

Sehemu nyingine ya makala hiyo inamnukuu mama mmoja, ambaye mtoto wake ana utapiamlo mkubwa akielezea jinsi alivyokata tamaa kwa kusema: "Mwanangu hataongezeka uzito hata kidogo. Kila tunapompima haongezeki kilo, tunampima kwa gramu. Kaka zake wakubwa wamelazimika kwenda vitani na wanahangaika huku na huku wakiwa na aina tofauti za bunduki."