Mapigano mashariki mwa DRC yazidisha mateso ya Waislamu, Swala ya Tarawih yasitishwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123396-mapigano_mashariki_mwa_drc_yazidisha_mateso_ya_waislamu_swala_ya_tarawih_yasitishwa
Baraza Kuu la Waislamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeamua kusimamisha Swala ya Tarawih katika miji ya mashariki inayokaliwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 02, 2025 03:59 UTC
  • Mapigano mashariki mwa DRC yazidisha mateso ya Waislamu, Swala ya Tarawih yasitishwa

Baraza Kuu la Waislamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeamua kusimamisha Swala ya Tarawih katika miji ya mashariki inayokaliwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.

Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu tawi la Bukavu, Sheikh Yassin Kabongo Mukoko, amesema viongozi wa dini wametoa fatwa ya kusitishwa Swala za Tarawih misikitini, kwa sababu hali ya usalama nchini hairuhusu raia kutoka nje nyakati za usiku.

Baraza hilo limewataka Waislamu wanaoishi karibu na misikiti kuchanganya Swala ya Maghrib na Isha na kurejea majumbani mwao kabla giza halijaingia.

Vilevile limewataka Waislamu ambao nyumba zao ziko mbali na misikiti kukaa katika maeneo yao na kuswali humo ili kuepuka mauaji.

Ramadhani ya mwaka huu inasadifiana na vita vya ndani ambavyo vinaendelea kwa wiki kadhaa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kati ya waasi wa M23 na vikosi vya jeshi la taifa, ambavyo bado havijaweza kuzuia kusonga mbele wapiganaji wa kundi hilo la waasi.

Waislamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanatambuliwa kuwa miongoni mwa jamii za wachache, na wanakadiriwa kuwa milioni 10, inayowakilisha 15% ya jumla ya watu wapatao milioni 77 wa nchi hiyo.

Takwimu zilizochapishwa na Jumuiya ya Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu zinasema kuwa, idadi ya Waislamu nchini Kongo imepungua kutoka milioni 17 hadi milioni 10 katika miongo ya hivi karibuni kutokana na mateso, umaskini, ujinga, kutengwa kwa makusudi, kampeni za wamisionari wa Kikristo na kadhalika.