Uganda yatuma wanajeshi zaidi DRC, huku mzozo ukiendelea
Jeshi la Uganda limethibitisha kutuma wanajeshi wake katika mji mwingine kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupambana na makundi yenye silaha, huku kukiwa na hofu kuwa mzozo mkali unaoendelea DRC unaweza kuingia katika vita vikubwa.
Felix Kulayigye msemaji wa wizara ya ulinzi na masuala ya kijeshi nchini Uganda amenukuliwa akisema kuwa: Majeshi yetu yameingia katika mji wa Mahagi na tunaudhibiti.
Kupelekwa kwa wanajeshi hao kuliombwa na jeshi la Congo kufuatia madai ya mauaji ya raia yaliyofanywa na kundi la wanamgambo linalojulikana kama Cooperative for the Development of Congo (Codeco), alisema, bila kutoa maelezo zaidi.
Mahagi iko katika mkoa wa Ituri, ambao unapakana na Uganda, ambako watu wasiopungua 51 waliuawa Februari 10 na watu wenye silaha wenye mafungamano na Codeco, kwa mujibu wa vyanzo vya kibinadamu na vya ndani.
Codeco inadai inatetea maslahi ya jamii ya Lendu, hasa inayoundwa na wakulima, dhidi ya jamii ya Hema, hasa wafugaji.
Uganda tayari ina maelfu ya wanajeshi katika maeneo mengine ya Ituri chini ya makubaliano na serikali ya Congo.
Mwezi uliopita, Uganda ilitangaza kuwa wanajeshi wake "wamechukua udhibiti" wa mji mkuu wa jimbo hilo, Bunia.
Wakati huo huo, Baraza Kuu la Waislamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limeamua kusimamisha Swala ya Tarawih katika miji ya mashariki inayokaliwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.
Inaelezwa kuwa, viongozi wa dini wametoa fat'wa ya kusitishwa Swala za Tarawih misikitini, kwa sababu hali ya usalama nchini huumo hairuhusu raia kutoka nje nyakati za usiku.