Rwanda: Serikali ya Uingereza imevunja uaminifu
Serikali ya Rwanda imeishutumu Uingereza kwa kile ilichokita kuwa kuvunja uaminifu na kuchukua hatua zisizo na msingi dhidi ya Kigali, na imeitaka serikali ya Uingereza iilipe Rwanda kiasi cha pauni milioni 50 chini ya mpango wa Ushirikiano wa Wahamiaji na Maendeleo ya Kiuchumi ambao haupo kwa sasa.
Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya Rwanda, ameikosoa Uingereza kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake, akisema Rwanda ilikubali kutochukua malipo hayo kwa kuzingatia uaminifu na imani iliyokuwepo kati ya mataifa hayo mawili.
Hata hivyo, Makolo anasema imani hii imekiukwa kupitia hatua za hivi karibuni za Uingereza, ikiwa ni pamoja na kusimamisha misaada kwa Rwanda na kutoa matamshi mabaya Bungeni.
"Uingereza iliitaka Rwanda kutodai malipo kwa kuzingatia uaminifu na nia njema iliyopo kati ya mataifa yetu mawili," Makolo alichapisha taarifa kwenye mtandao wa X.
"Hata hivyo, Uingereza imevunja imani hii kupitia hatua zisizo na msingi za kuilazimisha Rwanda kuhatarisha usalama wa "taifa letu". Rwanda pia imelaani kile ilichosema ni maoni mabaya yaliyotolewa Bungeni na Lord Collins, Waziri wa Uingereza wa masuala ya Afrika.
Mzozo kati ya nchi hizo mbili umeibuka baada ya Waziri wa Mambo ya Nje David Lammy kusitisha msaada wa Uingereza kwa Rwanda wiki iliyopita, akisema ni kutokana na Rwanda kuunga mkono kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Rwanda imekanusha vikali madai hayo, ikiishutumu Uingereza kwa kuendeleza hadithi za uongo na kudhoofisha juhudi za amani za kikanda.