Umoja wa Mataifa: Waasi wa M23 wawateka wagonjwa 130 mashariki mwa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123498-umoja_wa_mataifa_waasi_wa_m23_wawateka_wagonjwa_130_mashariki_mwa_drc
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, wapiganaji wa M23 wamewateka karibu watu 130 kutoka hospitali za mji wa Goma wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, unaodhibitiwa na waasi hao.
(last modified 2025-03-05T00:41:49+00:00 )
Mar 05, 2025 00:41 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Waasi wa M23 wawateka wagonjwa 130 mashariki mwa DRC

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, wapiganaji wa M23 wamewateka karibu watu 130 kutoka hospitali za mji wa Goma wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, unaodhibitiwa na waasi hao.

Umoja wa Mataifa umesema katika taarifa yakke kwamba, wiki iliyopita M23 iliwachukua watu 116 kutoka hospitali ya Ndosho mjini Goma na 15 wengine kutoa hospitali ya Heal Afrika, kwa madai kuwa wao ni sehemu ya jeshi la Kongo au wanamgambo wanaoiunga mkono serikali.

Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani amesema katika taarifa kuwa ofisi hiyo ina wasiwasi mkubwa kuhusu usalama na hali ya kiafya ya wagonjwa hao waliotekwa na M23.

"Inasikitisha sana kwamba M23 inawateka wagonjwa kutoka vitanda vya hospitali katika uvamizi ulioratibiwa na kuwaweka bila mawasiliano katika maeneo yasiyojulikana," Shamdasani amesema, akitaka waachiliwe mara moja.

Kongo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi wanaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo la waasi.

Takriban watu 7,000 wameuawa mashariki mwa Kongo tangu mwezi wa Januari na karibu watu nusu milioni waliachwa bila makazi baada ya kambi 90 za wakimbizi kuharibiwa katika mapigano hayo, kulingana na serikali.

Vikwazo vya kimataifa, uchunguzi upya wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Afrika yameshindwa kusitisha kusonga mbele kwa waasi, ambao wameiteka miji mikuu miwili ya mashariki mwa Kongo, Goma na Bukavu.

Wakati huo huo, hali ya kibiinadamu mashariki mwa DRC inaelezwa kuwa imezidi kuwa mbaya kutokana na vita na mapigano katikka maeneo hayo.