Wahamiaji 349 walizuiwa kuendelea na safari katika pwani ya Libya wiki iliyopita
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema jana Jumanne kwamba wahamiaji 349 walizuiwa kuendelea na safari nje ya pwani ya Libya wiki iliyopita.
Katika taarifa yake hiyo ya jana, IOM imesema: "Kuanzia Februari 23 hadi Machi 1, wahamiaji 349 walikamatwa na kurejeshwa Libya, wakiwemo wanawake 21 na watoto sita."
Kwa mujibu wa shirika hilo la kimataifa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, wahamiaji 4,204 wameshakamatwa na kurejeshwa Libya na wahamiaji 80 wameshafariki dunia katika juhudi zao za kuvuka mawimbi makali ya Bahari ya Mediterania kujaribu kuelekea barani Ulaya.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya, Emad al-Tarabelsi alisema hivi karibuni kwamba nchi yake inaweza kuamua "kuwafukuza kwa lazima wahamiaji haramu" kama jamii ya kimataifa itashindwa kuunga mkono juhudi za kurejeshwa makwao kwa hiari.
Wahamiaji haramu wanakumbwa na majanga mengi huko Libya kiasi kwamba, katikati ya mwezi uliopita wa Februari, Mamlaka za Libya ziligundua miili ipatayo 50 kwenye makaburi mawili ya umati katika jangwa la kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Hayo yalihesabiwa akuwa ni maafa ya karibuni zaidi yaliyohusisha watu wanaopigania kufika Ulaya kupitia nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Kurugenzi ya usalama ya Libya ilieleza katika taarifa yake kwamba kaburi moja la umati lililopatikana katika shamba lililoko kusini mashariki mwa mji wa Kufra lilikuwa na miili 19. Mabaki ya miili hiyo yalichukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Mohamed al-Fadeil, mkuu wa idara ya usalama mjini Kufra alisema, kaburi la pili la umati lenye karibu miili 30 nalo pia liligunduliwa katika mji huo baada ya maafisa wa mamlaka husika kuvamia kituo kimoja cha wahamiaji haramu.
Al Fadeli ameongeza kuwa kwa mujibu wa maelezo ya walionusurika, karibu watu 70 walizikwa katika eneo hilo. Maafisa husika wangali wanaendelea kufanya uchunguzi.