Ghala la silaha za Daesh lanaswa Sirte, Libya
Vikosi vya jeshi la Libya vimegundua na kunasa karakana moja ya kuzalisha mabomu ya kutega ardhini, mada za miripuko na ghala lililokuwa na silaha za aina mbalimbali mali ya kundi la kigaidi la Daesh huko mashariki mwa mji wa Sirte nchini humo.
Jeshi la Libya limetangaza kuwa limenasa ghala lililosheheni silaha za aina mbalimbali na karakana ya kuzalisha mabomu ya kutega ardhini na mada za miripuko mali ya kundi la Daesh. Makombora ya kutungulia vifaru na silaha zingine ni kati ya zana za kijeshi zilizonaswa na jeshi la Libya huko Sirte.
Mapigano makali kati ya vikosi vya jeshi la Libya na wanamgambo wa Daesh yalianza tangu zaidi ya miezi miwili iliyopita huko Sirte na katika mapigano hayo, wanajeshi wa Libya walifanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa Daesh katika maeneo ya kistratejia ya mji huo.
Jumapili iliyopita pia jeshi la Libya lilitangaza kuwa vikosi vyake vimedhibiti moja kati ya vituo vikubwa vya kutengenezea mabomu vya Daesh katika eneo la al Sawara.
Katika upande mwingine serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imesisitiza kuwa uingiliaji wa Ufaransa mashariki mwa nchi hiyo ni nje ya uendeshaji wa serikali na baraza la kisiasa la Libya na kwamba serikali hiyo haina taarifa kuhusu uingiliaji huo wa Ufaransa.