Uingereza yakataa kuilipa Rwanda fidia baada ya kufuta mkataba wa wahamiaji
Serikali ya Uingereza imekataa kuilipa Rwanda fidia baada ya kufuta mkataba wa wahamiaji kati ya nchi hizo mbili.
Jumatatu, Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya Rwanda, alisema kuwa Uingereza iliomba Rwanda "kuachana kimyakimya" na malipo yaliyosalia – yanayoripotiwa kufikia pauni 50 milioni sawa na dola milioni 64 za Marekani.
Hata hivyo, Rwanda sasa inaitaka Uingereza kulipa kiasi kilichosalia ambacho inadai inastahili kulipwa, ikiituhumu Uingereza kwa kuvunja uaminifu kwa kusimamisha baadhi ya misaada kwa nchi hiyo.
Katika taarifa, msemaji wa serikali ya Uingereza amesema kuwa "hakutakuwa na malipo zaidi yanayohusiana na sera hii. "
Mvutano kuhusu malipo yanayohusiana na mpango wa Rwanda unakuja baada ya serikali ya Uingereza kutangaza mwezi uliopita kuwa itasitisha misaada kwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Serikali ya Uingereza iliamua kupunguza misaada baada ya kuishutumu Rwanda kuwa inaunga mkono waasi wa M23, kundi la waasi ambalo limechukua sehemu kubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika uasi wenye umwagaji damu.
Makolo alisema Jumatatu kuwa upunguzaji huo wa misaada ni "hatua za adhabu zisizo na msingi zinazolenga kuilazimisha Rwanda kukubali kuhatarisha usalama wake wa kitaifa".
Rwanda mara kwa mara imekanusha kuunga mkono kundi la waasi la M23, lakini hivi karibuni imekuwa na msimamo mkali zaidi, ikisema imelazimika kuchukua hatua za kukabiliana na "tishio la kimsingi" linalosababishwa na wanamgambo karibu na mipaka yake.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa hapo awali walikadiria kuwa kati ya wanajeshi 3,000 na 4,000 wa Rwanda wako katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Makolo amesema sasa Rwanda itafuatilia malipo yaliyosalia yanayohusiana na mkataba wa wahamiaji kwa msingi kuwa Uingereza ilikuwa "imefungwa kisheria" kuutekeleza.