Sudan Kusini kuzishawishi UN na IGAD zikubali mabadiliko ya uongozi
Serikali ya umoja wa kitaifa ya Sudan Kusini imemteua Makamu mpya wa Rais aliyechukua nafasi ya Riek Machar kuufafanulia Umoja wa Mataifa sababu za kufanyika mabadiliko ya uongozi ndani ya chama cha upinzani cha SPLM-IO.
James Wani Igga, Makamu wa Pili wa Rais wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika amesema Rais Salva Kiir amemteua Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa sasa kuongoza ujumbe wa upinzani kwenda mjini New York makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuushawishi umoja huo uunge mkono serikali ya sasa inayoongozwa na yeye na Kiir. Baadaye Deng Gai anatazamiwa kuelekea Khartoum nchini Sudan kukutana na viongozi wa jumuiya ya kieneo ya IGAD kujadili suala hilo la uongozi mpya.
Haya yanajiri katika hali ambayo, Riek Machar anasisitiza kuwa angali Makamu wa Rais wa nchi hiyo na kwamba karibuni hivi atarejea mjini Juba kuendelea kushikilia wadhifa wake.
Haya yanajiri siku tatu baada ya Samuel Makuei, Waziri wa Habari wa Sudan Kusini kukanusha taarifa kuwa Rais Salva Kiir ndiye aliyemteua Taban Deng Gai kujaza nafasi ya Riek Machar na kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, uteuzi huo ulifanywa na chama chenyewe cha upinzani cha SPLM.
Umoja wa Mataifa umemuonya Rais Salva Kiir kuhusu uteuzi wa kisiasa unaofanyika katika kipindi cha sasa cha kushtadi mgogoro wa kisiasa nchini Sudan Kusini. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq alisema kuwa uteuzi wa aina yoyote wa viongozi wa kisiasa huko Sudan Kusini unapaswa kuoana na makubaliano ya amani yaliyofikiwa yapata miaka miwili iliyopita kati ya pande hasimu nchini humo kwa shabaha ya kuhitimisha vita vya ndani.
Machafuko mapya mjini Juba yamepelekea kuuawa watu wasiopungua 300 hadi sasa na kutishia kuzuka tena vita vya ndani huko Sudan Kusini.