Mali yasitisha vibali vya uchimbaji madini kwa wageni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123566-mali_yasitisha_vibali_vya_uchimbaji_madini_kwa_wageni
Waziri wa Usalama na Ulinzi wa Raia wa Mali, Daoud Aly Mohammedine ametangaza rasmi kwamba: Vibali vyote vya uchimbaji madini nchini Mali vilivyotolewa kwa watu wenye uraia wa kigeni vimesitishwa kwa amri ya Rais Assimi Goïta wa Mali.
(last modified 2025-03-06T06:26:46+00:00 )
Mar 06, 2025 06:26 UTC
  • Mali yasitisha vibali vya uchimbaji madini kwa wageni

Waziri wa Usalama na Ulinzi wa Raia wa Mali, Daoud Aly Mohammedine ametangaza rasmi kwamba: Vibali vyote vya uchimbaji madini nchini Mali vilivyotolewa kwa watu wenye uraia wa kigeni vimesitishwa kwa amri ya Rais Assimi Goïta wa Mali.

Hatua hii inafuatia kuporomoka mara mbili kwa maeneo ya uchimbaji dhahabu. Tukio la kwanza, lililotokea Februari 15 magharibi mwa Mali, lilisababisha karibu vifo 50, wakati la pili, lililotokea Januari 29 kusini magharibi mwa Mali, liligharimu takriban maisha kumi.

Kwa mujibu wa waziri huyo ambaye alizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Bamako, Rais Assimi Goïta wa Mali ameiamrisha serikali kuimarisha hatua za kuzuia majanga ya kibinadamu na mazingira nchini Mali.

Waziri wa Usalama na Ulinzi wa Raia wa Mali pia amesema kuwa, Rais Goïta pia ameamua kutengua uteuzi wa maafisa wa utawala waliohusika moja kwa moja na kutokea kwa matukio haya.

Mashirika ya kigeni yanajali faida binafsi tu, yanaangamiza kabisa mazingira

 

Kuna uchimbaji mkubwa sana wa kiholela wa madini nchini Mali na katika nchi nyingine za Afrika ikiwemo nchi jirani ya Senegal.

Mashirika ya kigeni yanafanya uchaguzi mkubwa wa mazingira na kuangamiza rasilimali nyingi za nchi za Afrika wakati wa uchimbaji wa madini.

Mwaka jana serikali ya Senegal ilipiga marufuku kwa muda wa miaka mitatu  shughuli za uchimbaji madini kwenye ukingo wa mto ambao ni sehemu ya mpaka wake na nchi ya Mali kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kulinda afya za wenyeji.

Mto Faleme, ukingo mkuu wa Mto Senegal, ni maarufu hivi sasa kwa uchafuzi mkubwa wa mazingira na matumizi makubwa ya kemikali katika utitiri wa migodi ya dhahabu kutokana na kutodhibitiwa uchimbaji wake.