Ufaransa yazidi kutimuliwa Afrika, yakabidhi kambi mbili kwa Senegal
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123620-ufaransa_yazidi_kutimuliwa_afrika_yakabidhi_kambi_mbili_kwa_senegal
Kambi mbili kati ya tano za jeshi la mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa nchini Senegal zilikabidhiwa rasmi kwa serikali ya nchi hiyo jana Ijumaa. Hiyo ni hatua ya kwanza kuelekea kutimuliwa kikamilifu wanajeshi wa Ufaransa nchini humo.
(last modified 2025-03-08T00:55:15+00:00 )
Mar 08, 2025 00:55 UTC
  • Ufaransa yazidi kutimuliwa Afrika, yakabidhi kambi mbili kwa Senegal

Kambi mbili kati ya tano za jeshi la mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa nchini Senegal zilikabidhiwa rasmi kwa serikali ya nchi hiyo jana Ijumaa. Hiyo ni hatua ya kwanza kuelekea kutimuliwa kikamilifu wanajeshi wa Ufaransa nchini humo.

Kambi hizo za kijeshi za Maréchal na Saint-Exupéry, haziko mbali na bandari ya Dakar na zimerejeshwa rasmi kwa serikali ya Senegal.

Tangu alipoingia madarakana mwezi Aprili mwaka jana, Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal amekuwa akitangaza wazi kuwa anataka kurekebisha uhusiano wa nchi yake dola la kikoloni la Ufaransa ambalo linafanya unyonyaji mkubwa dhidi ya makoloni yake ya zamani barani Afrika. Mwezi Novemba mwaka jana Rais Diomaye Faye aliviambia vyombo vingi vya habari kwamba, karibuni hivi wanajeshi wa mkoloni Ufaransa hawatakuweko tena nchini Senegal.

Kambi tatu za kijeshi za Ufaransa zilizobakia huko Senegal nazo zitafungwa na wanajeshi wa nchi hiyo ya Ulaya watatimuliwa, lakini tarehe hasa haijatangazwa. Hivi sasa kuna zaidi ya wanajeshi 200 wa Ufaransa na familia zao huko Camp Geille ambayo ni kambi kubwa zaidi kati ya kambi tano za kijeshi za Ufaransa nchini Senegal.

Hatua hii imekuja baada ya ile ya siku ya Alkhamisi, Februari 20, 2025, wakati wanajeshi wa mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa walipotimuliwa katika kambi yao pekee ya kijeshi nchini Ivory Coast. Takriban wanajeshi elfu moja wa Ufaransa walikuweko katika kambi iitwayo "Port Bouet" chini ya kivuli cha kukabiliana na ugaidi na kupambana na magenge yenye itikadi kali. Mwezi Disemba 2024, Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast alitangaza kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa nchini mwake. Hatua hiyo imechukuliwa kama sehemu ya kuendeleza wimbi la kufukuzwa wanajeshi wa Ufaransa barani Afrika na kupunguza uwepo wa kijeshi wa Paris barani humo.