Ujangili wakithiri A/Kusini, vifaru 420 wawindwa kinyume cha sheria
Waziri wa Misitu, Uvuvi na Mazingira wa Afrika Kusini, Dion George, ametoa taarifa rasmi na kusema kuwa vifaru 420 waliuliwa kinyume cha sheria kwa ajili ya pembe zao nchini Afrika Kusini mwaka 2024, ingawa idadi hiyo iko chini ya ile ya mwaka juzi, 2023, ambapo vizuri 499 waliuliwa na majangili kwa ajili ya vipusa.
Akitangaza takwimu za ujangili za kila mwaka, Waziri George amebainisha kuwa, vifaru 320 waliwindwa kinyume na sheria katika hifadhi za serikali na 100 wengine waliuawa kwenye mbuga, hifadhi au mashamba ya watu binafsi.
Waziri huyo amesema kuwa, kupungua idadi hiyo ikilinganishwa na mwaka juzi kunatokana na kuimarishwa hatua za kukabiliana na ujangili. "Upimaji wa polygraph ya wafanyakazi unaendelea katika Hifadhi ya Taifa ya Kruger ili kuleta uadilifu na kuzuia vitendo vya ujangili. Hadi sasa, uchunguzi ambao umetokana na matokeo upimaji wa polygraph umepelekea kuchukuliwa hatua za kinidhamu wafanyakazi wawili katika Huduma za Mgambo ambao wamepatikana na hatia za kushiriki kwenye ujangili."
Vilevile amesema: Ushirikiano na wadau mbalimbali umewasaidia maafisa wa forodha na wasimamizi wa sheria kuwagundua majangili na kudhibiti magendo ya pembe za vifaru.
Afrika Kusini inaendesha Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Wanyamapori, ikifanya kazi kwa karibu na tawala za nchi zinazopitishiwa nyara hizo na nchi ambazo vipusa hivyo vinapelekwa.
Waziri George pia amesema: "Afrika Kusini itaendelea kujitolea katika mapambano dhidi ya ujangili wa vifaru na ninaamini kwamba uimarishaji upya wa mikataba yetu na itifaki za kiutendaji na nchi muhimu inapaswa kuwa lengo letu kwa mwaka huu wa 2025."