Ethiopia yaanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya al-Shabab nchini Somalia
Jeshi la anga la Ethiopia limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab katika Mkoa wa Shabelle ya Kati nchini Somalia. Mashambulizi hayo ya anga yametokea baada ya kutiwa saini mkataba wa usalama kati ya Somalia na Ethiopia mwezi uliopita.
"Hakuna mashambulizi ya anga yanayoweza kufanyika nchini Somalia bila ya serikali kujua," Waziri wa Ulinzi wa Somalia Abdulkadir Mohamed Nur amenukuliwa akisema hayo na kuongeza kuwa, jeshi la ulinzi la Somalia pia limeshiriki katika operesheni hiyo.
Waziri Mohamed Nur amegusia pia namna ushirikiano wa usalama kati ya Somalia na Ethiopia ulivyoongezeka na kusema kuwa, Mkataba wa Ankara ndiyo marejeo ya juhudi zao za pamoja za kupambana na magaidi wa al-Shabab.
Mashambulizi hayo yamefanyika ikiwa ni operesheni ya kwanza ya anga ya Ethiopia katika eneo hilo kwenye miaka ya hivi karibuni. Hivi karibuni Somalia iliruhusu vikosi vya Ethiopia vijiunge na juhudi za Umoja wa Afrika (AU) za kuleta amani na utulivu wa kudumu nchini Somalia.
Eneo la Shabelle ya Kati kwa muda mrefu limekuwa kitovu cha mapigano kati ya al-Shabab na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na wanajeshi wa AU. Kujiunga Ethiopia na operesheni za kupambana na genge la kigaidi la al-Shabab kumekuja baada ya miezi kadhaa za mvutano baina ya nchi mbili ambao ulihitimishwa kwa kutiwa saini Mkataba wa Ankara na kufikiwa makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi baina ya nchi hizo mbili jirani.
Makamanda wa kijeshi wanchi hizo mbili walikutana katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu mwezi Februari na kukubaliana kuimarisha operesheni za pamoja dhidi ya magaidi wa al Shabab.