Waziri wa Ulinzi wa Sudan: Jeshi limepiga hatua kubwa dhidi ya RSF
Waziri wa Ulinzi wa Sudan, Yassin Ibrahim, amesema kuwa jeshi la nchi hiyo limepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Yassin Ibrahim ameongeza kuwa, athari za operesheni za kijeshi zinazofanyika hivi sasa zitaonekana katika siku za usoni, na Sudan itarejesha katika usalama na utulivu wake.
Amesema kuwa vita nchini Sudan vilizuka kutokana na mipango ya nje, na kwamba RSF inatekeleza nafasi ya mchezaji tu, akisisitiza kuwa "vita vinavyoendelea hivi sasa nchini Sudan ni vita vya "kufa au kupona."
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Jeshi la Sudan huko Al-Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, vimesema kwamba askari wa nchi kavu wamefanya operesheni kubwa ambayo imesababisha hasara kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka.
Huko Darfur Kusini, jeshi la Sudan limeripoti kuwa kuna mvutano na migogoro ndani ya safu ya Vikosi vya Msaada wa Haraka katika mhimili wa mji wa Nyala, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kusini.
Katika wiki chache zilizopita, RSF imepoteza eneo muhimu kwa jeshi la serikali katika majimbo ya Khartoum, al-Jazira, Kordofan Kaskazini, White Nile, Sennar na Blue Nile.