UNICEF asilimia 50 ya Watanzania ni watoto; vijana ni 72%
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123782-unicef_asilimia_50_ya_watanzania_ni_watoto_vijana_ni_72
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetilia mkazo msimamo wake wa kuwasaidia watoto nchini Tanzania ili kuwawwezesha wasichana wanaobaleghe kupata huduma za elimu, afya na lishe nzuri.
(last modified 2025-03-11T08:06:08+00:00 )
Mar 11, 2025 08:06 UTC
  • UNICEF asilimia 50 ya Watanzania ni watoto; vijana ni 72%

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetilia mkazo msimamo wake wa kuwasaidia watoto nchini Tanzania ili kuwawwezesha wasichana wanaobaleghe kupata huduma za elimu, afya na lishe nzuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell ametoa ahadi hiyo alipotembelea mkoa wa Songwe kukagua programu za elimu na afya kwa watoto na wasichana wanaobaleghe. Programu hizo zinafadhiliwa na UNICEF na ambazo zinakusudia kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya watoto nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UNICEF, shirika hilo la Umoja wa Mataifa linashirikiana na serikali ya Tanzania na washirika wake katika uendeshaji wa sera za uwekezaji unaosaidia watoto na vijana hasa wasichana kuboresha upatikanaji wa elimu, huduma za afya na lishe kwa jamii na kupunguza mimba za utotoni.

Watoto Tanzania wanaunda asilimia 50 ya watu wote

 

Russell ambaye ziara yake ya siku tatu nchini Tanzania imemalizika leo Jumanne ameongeza kuwa, asilimia 50 ya Watanzania ni watoto na asilimia 72 ni vijana. Amebainisha kuwa, UNICEF ina dhamira thabiti ya kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania za kuwekeza kwa manufaa ya watoto hao.

Amesema: "Tanzania imeonesha kuwa kuwekeza kwa ajili ya watoto na vijana hakuhusiani tu na maisha yao ya baadaye bali ni kuhusu mustakabali wa taifa zima la Tanzania." Aidha amesema: "Tanzania ni mfano muhimu wa kuigwa kwani imethibitisha kivitendo kwamba, kuwapa watoto kipaumbele ni jambo sahihi na la busara."

Juzi Jumapili, Russell alikutana na wasichana waliobaleghe na wabunifu wa kike katika mpango unaoungwa mkono na UNICEF jijini Dar es Salaam ili kuwapa vijana ujuzi wa kidijitali wa kuwawezesha kushughulikia changamoto nyingi ndani ya maisha yao.