Kongo yashindwa kuzuia mlipuko wa ugonjwa wa Mpox
Wiki sita baada ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda kuteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, eneo hilo linakabiliwa na hali mbaya katika mapambano yake dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa mpox.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara kwa mara imekuwa ikiathiriwa na milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na virusi huku kitovu cha maambukizi kikiwa mashariki mwa nchi hiyo.
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika kimesema wagonjwa wa Mpox zaidi ya 600 wametoroka katika hospitali mbalimbali kufuatia kushtadi mapigano ya waasi wa M23.
Afrika CDC imesema: Wiki jana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa na ongezeko la asilimai 31 ya wagonjwa wa ugonjwa wa Mpox na hivyo kuifanya idadi jumla ya wagonjwa kufikia 16,255.
Dr Serge Munyahu Cikuru, Afisa anayesimamia eneo la afya la Miti Murhesa katika jimbo la Kivu Kusini anasema: "Hali ya mambo ni ngumu sana, ukosefu wa usalama umevuruga kila kitu."
Amesema, ni vigumu sana kuwasaka na kuwabaini watu wenye maambukizi ya Mpox kutokana na hali ya mchafukoge na mapigano.
Mwezi jana Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitahadharisha kuwa virusi vya Mpox aina ya Clade 1b vinaendelea kuenea duniani.