Niger yajitoa rasmi katika Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa, Francophone
Niger imejiondoa rasmi katika Jumuiya ya Kimataifa ya nchi zinazozungumza Kifaransa (OIF) au Francophone sambamba na juhudi zinazoendelea kufanywa na taifa hilo la Afrika Magharibi za kuvunja uhusiano na kujitenga na mkoloni wake wa zamani, Ufaransa.
Baraza la Kudumu la wanachama 88 wa OIF lilisimamisha uanachama wa Niger mwezi Desemba 2023 miezi kadhaa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Julai mwaka huo ambayo yalimuondoa madarakani rais wa zamani Mohamed Bazoum. Uamuzi huo wa OIF ulichukuliwa ili kuushinikiza uongozi mpya wa kijeshi kurejesha utawala wa katiba nchini Niger.
Baraza hilo la Jumuiya ya Kimataifa ya nchi zinazozungumza Kifaransa lilitangaza kuwa litaendeleza ushirikiano na Niger katika miradi ambayo inanufaisha raia moja kwa moja na kuchangia katika kurejesha demokrasia katika koloni hilo la zamani la Ufaransa.
Hata hivyo tangu iliposhika hatamu za uongozi wa nchi, serikali ya kijeshi ya Niger, inayojulikana kama Baraza la Kitaifa la Kulinda Nchi, imechukua hatua kadhaa za kukata uhusiano na Paris, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa na vituo vya kijeshi nchini humo.../