Jeshi la Uganda: Tumeua waasi zaidi ya 200 mashariki ya DRC
(last modified Sun, 23 Mar 2025 02:47:45 GMT )
Mar 23, 2025 02:47 UTC
  • Jeshi la Uganda: Tumeua waasi zaidi ya 200 mashariki ya DRC

Jeshi la Uganda limetangaza habari ya kuwaua mamia ya wapiganaji wa kundi la waasi wa CODECO baada ya kushambulia kambi ya jeshi la Uganda katika mpaka wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Msemaji wa jeshi la Uganda, Chris Magezi amesema mamia ya wapiganaji wa CODECO walishambulia kituo cha Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) katika eneo la Fataki, katika jimbo la Ituri, mashariki ya DRC Jumatano na Alkhamisi.

Hata hivyo kundi hilo la wanamgambo wanaobeba silaha mashariki mwa DRC limepinga vikali madai hayo ya kuvamia kambi ya jeshi la Uganda.

Msemaji wa jeshi la Uganda amebainisha kuwa, askari wa Uganda wamefanikiwa kuwaangamiza wapiganaji 242 wa kundi la waasi wa CODECO, katika operesheni ya ulipizaji kisasi.  

CODECO ni muungano wa makundi kadhaa ya waasi na ni miongoni mwa makundi mengi ya wanamgambo wanaopigania ardhi na rasilimali katika eneo lenye utajiri wa madini la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wanamgambo wa CODECO mashariki mwa DRC

Umoja wa Mataifa unasema baadhi ya mashambulizi yanayotekelezwa na CODECO yanaweza kujumuisha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Haya yanajiri huku waasi wa M23 wakiendeleza mashambulizi makubwa huko Mashariki mwa Congo DR tangu mwanzoni mwa huu wa 2025, na kudhibiti maeneo na miji mengi, ikiwa ni pamoja na Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Inakadiriwa kuwa watu milioni 1 wameyakimbia makazi yao, na wengine 7,000 wameuawa tangu mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na mapigano hayo.