Nigeria yalaaniwa kwa kukandamiza waandamanaji wa Siku ya Quds
(last modified Sun, 30 Mar 2025 11:12:08 GMT )
Mar 30, 2025 11:12 UTC
  • Nigeria yalaaniwa kwa kukandamiza waandamanaji wa Siku ya Quds

Baraza la Uratibu wa Tablighi ya Kiislamu la Iran limetoa taarifa ya kulaani ukandamizaji waliofanyiwa Waislamu wa Nigeria wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds na kuandika: "Ukandamizaji na kumwagwa damu za waandamanaji wa Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Nigeria na kuuawa shahidi kidhulma Waislamu 18 waliokuwa kwenye saumu ya Ramadhani kunaonesha hofu ya watawala wa Nigeria kuhusu mwamko wa Waislamuj na nafasi ya kiistratijia ya Siku ya Kimataifa ya Quds duniani."

Katika taarifa yake hiyo, baraza hilo limeongeza kuwa, maadui wa Uislamu ambao wametambua umuhimu wa Siku ya Quds kuwa ni kitovu na nguzo ya kupambana na uvamizi, kwa mara nyingine tena wamejaribu kuzima moto wa mwamko wa Waislamu kwa kutumia nguvu na ukandamizaji wa kikatili. Lakini wasichojua maadui hao ni kwamba damu iliyomwagwa kinyume na haki ya watu waliokuwa ndani ya funga ya Ramadhani huko Nigeria, Ghaza, na Lebanon itaendelea kwa upande mmoja kuwa na taathira maradufu katika njia ya kutokomeza dhuluma na uhalifu duniani.

Baraza la Uratibu wa Tablighi ya Kiislamu la Iran mbali na kulaani vikali jinai hiyo na kutangaza mshikamano na wananchi wanaodhulumiwa wa Nigeria, limesisitiza kuwa, njia bora ya kukomboa Quds itaendelea kwa nia na imani thabiti zaidi kuliko huko nyuma.

Baraza hilo limesisitiza kuwa damu ya mashahidi wa Nigeria, kama kiungo chenye kuendelea katika kambi ya Muqawama, inaimarisha mapambano na inathibitisha kwamba kuadhimisha Siku ya Quds si tukio la muda mfupi, bali ni mkakati endelevu dhidi ya mfumo wa utawala na uvamizi.

Siku ya Ijumaa, makumi ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria waliandamana kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds ili kutangaza mshikamano na Palestina, lakini ghafla askari polisi walivamia na kumwaga damu za Waislamu hao.