Viongozi wa upinzani Kenya wadai, Rais Ruto na washirika wake wanataka kuiteka IEBC
(last modified Wed, 02 Apr 2025 06:40:17 GMT )
Apr 02, 2025 06:40 UTC
  • Viongozi wa upinzani Kenya wadai, Rais Ruto na washirika wake wanataka kuiteka IEBC

Viongozi wa upinzani nchini Kenya wamepinga mchakato unaoendelea wa kuunda upya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), wakimshutumu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kwa kuvuruga mchakato huo.

Viongozi hao pia wamedai kuwa kuna kampeni za mapema na zisizo halali zinazoendeshwa na chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto na Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Bw Odinga.

Wakiongozwa na kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka, mkuu wa People’s Liberation Party, Martha Karua, na Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya, viongozi hao wamedai kuwa serikali ya Kenya Kwanza inapanga kudhibiti mchakato wa kuajiri makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wamesema mchakato wa uteuzi unavurugwa ili kuhakikisha kwamba watu waaminifu kwa Kenya Kwanza pekee ndio watakaoteuliwa kwa ajili ya nafasi hizo muhimu, jambo ambalo litatoa mwanya wa wizi wa kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Tunashangazwa na jinsi utawala wa Ruto ulivyojizatiti kudhibiti na kuelekeza mchakato wa uajiri wa makamishna wa IEBC kwa lengo la kuteka tume inayosimamia uchaguzi", amesema Martha Karua na kuongeza kuwa: “Huu ni mpango mchafu, ambao tunaamini unalenga kuiba kura katika uchaguzi mkuu ujao ili kuendeleza utawala wa Kenya Kwanza ambao tayari umepoteza imani ya Wakenya.” 

Akihutubia wanahabari katika Hoteli ya Serena jana Jumanne, Bi Karua alisema kuwa hadi sasa, “mchakato wa kuorodhesha majina umeacha nje Wakenya wenye sifa bora na uzoefu, kulingana na tathmini yetu ya waombaji zaidi ya 1,400 waliotuma maombi ya nafasi hizo.”

Viongozi hao wa upinzani pia wameliitaka Jopo la Uteuzi la IEBC kutojihusisha na vitendo vyovyote vya upendeleo ambavyo vinaweza kuhatarisha haki za uchaguzi nchini Kenya.