UNRWA yatahadharisha: Ukanda wa Gaza upo kwenye ukingo wa njaa
Philippe Lazaarini Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa kuzingirwa eneo hilo na utawala wa Kizayuni kunakwamisha misaada ya kibinadamu kuingia katika hilo; kwa hiyo wakazi wa eneo hilo wapo kwenye ukingo wa njaa.
Lazaarini ameashiria kurundikana misaada ya kibinadamu katika vivuko vya Gaza na kusema: 'Bidhaa mbalimbali za chakula zinaharibika huku muda wa matumizi ya dawa za matibabu ukimalizika.' Amesema mzingiro dhidi ya Gaza unapasa kuondolewa na vivuko kufunguliwa.
Shirika la UNRWA na taasisi nyingine za kimataifa mara kadhaa zimeitaka jamii ya kimataifa izuie kutokea maafa kamili ya binadamu huko Gaza na izidishe mashinikizo yake kwa utawala wa Kizayuni.
Wakati huo huo Mfuko wa Kuwahudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) pia umetangaza katika taarifa yake kuwa watoto katika Ukanda wa Gaza si tu wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na kushtadi mashambulizi ya Israel, bali wanakabiliwa na tishio la njaa, uhaba wa dawa za matibabu na kuambukizwa na magonjwa mbalimbali kutokana na kukosekana maji safi na salama ya matumizi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika muda wa siku mbili tu zilizopita, zaidi ya watoto 45 wa Kipalestina wameaga dunia.
Aidha jumla ya watoto 950 wameuawa shahidi huko Gaza tangu kuanza vita na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya eneo hilo.
Shirika la UNICEF pia limeitaja hali ya Gaza kuwa "ya maafa" na kutahadharisha kuwa kizazi chote kinakabiliwa na hatari ya kupoteza usalama, afya, elimu na matumaini.