Mamia ya familia zalazimika kukimbia baada ya RSF kushambulia vijiji Darfur, Sudan
(last modified Tue, 08 Apr 2025 09:42:59 GMT )
Apr 08, 2025 09:42 UTC
  • Mamia ya familia zalazimika kukimbia baada ya RSF kushambulia vijiji Darfur, Sudan

Mamia ya familia zimefurushwa kutoka vijiji viwili magharibi mwa Sudan baada ya mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF). Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).

IOM imeeleza katika taarifa hiyo: "familia zipatazo 530 zimefurushwa kutoka vijiji vya Abu Hamira na Al-Rakab katika Jimbo la Darfur Kaskazini kutokana na kuzidi kuwa mbaya hali ya usalama kati ya Aprili Mosi hadi 6".

Taasisi ya ndani iitwayo Abu Shouk Emergency Room imesema watu watatu, wakiwemo watoto wawili, walijeruhiwa jana Jumatatu katika shambulio la makombora lililofanywa na RSF katika moja ya vijiji hivyo.

Katika wiki za hivi karibuni, udhibiti wa maeneo wa RSF umekuwa ukipungua kwa kasi mkabala na jeshi la Sudan katika majimbo kadhaa, ikiwa ni pamoja na Khartoum, Al-Jazira, White Nile, Kordofan Kaskazini, Sennar, na Blue Nile.

Pande mbili za Jeshi la Sudan, SAF na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, RSF zimekuwa zikipigana vita tangu Aprili 2023 ambavyo vimeua zaidi ya watu 20,000 na kuwafanya wengine milioni 14 walazimike kuyahama makazi yao.

Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Hata hivyo utafiti wa wasomi wa Marekani unakadiria idadi ya vifo kuwa ni karibu 130,000.

Jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa zimetoa wito wa kusitishwa vita hivyo, zikitahadharisha kuhusu janga la kibinadamu linalokaribia kuikumba Sudan huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na hatari ya baa la njaa na vifo kutokana na uhaba wa chakula. Mzozo huo umeenea hadi kwenye majimbo 13 kati ya 18 ya Sudan.../