Sudan: RSF imeua raia wengine 32 El-Fasher, Darfur Kaskazini
Jeshi la Sudan limesema kwa uchache raia 32 wameuawa katika shambulio jipya la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko El-Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini.
"Wanamgambo (wa RSF) walitumia ndege nyingi zisizo na rubani huko El Fasher (Ijumaa), pamoja na mizinga kwa wakati mmoja kwenye shambulio hilo," Kamandi ya Kikosi cha 6 cha Jeshi la Sudan (SAF) imesema katika taarifa yake.
Idadi ya waliofariki dunia kwenye hujuma hiyo ni pamoja na wanawake 4 na watoto 10, huku watu wengine 17 wakijeruhiwa na kulazwa hospitalini, jeshi la Sudan limeeleza katika taarifa yake hiyo.
Kamati za Uratibu wa Mapambano huko El-Fasher zimethibitisha shambulio la RSF na kusema kuwa, droni na mizinga ililenga maeneo ya kaskazini na mashariki mwa jiji hilo.
Kikundi hicho kimewaomba wakazi kutoingia mitaani na barabarani kutokana na operesheni zinazoendelea za droni.

Kadhalika Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti habari ya kujiri shambulio la pili la RSF kwenye kambi ya wakimbizi ya Zamzam karibu na El-Fasher, ingawaje hakuna taarifa iliyotolewa ya waliouawa au kujeruhiwa. Mtandao huo umelaani matumizi ya silaha nzito katika shambulio hilo.
Sudan imekuwa katika mzozo mbaya unaotokana na uchu wa madaraka tangu katikati ya mwezi Aprili 2023. Hadi hivi sasa watu 29,683 wameripotiwa kuawaa kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Aidha vita vya Sudan vimewakosesha makazi zaidi ya watu milioni 15, ndani na nje ya nchi hiyo.