Buhari akanusha madai ya kuzuka mpasuko wa kidini Nigeria
Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria amekanusha madai kwamba serikali yake inafanya kila iwezalo kuleta mgawanyiko na matafaruku wa kidini nchini humo.
Garba Shehu, msemaji wa Rais Buhari amekosoa vikali makala iliyochapishwa na gazeti la Telegraph la Uigereza iliyodai kwamba serikali ya Abuja imepanda mbegu za mgawanyiko na kuzusha mpasuko mkubwa kati ya Waislamu na Wakristo wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika; na kusisitiza kuwa tuhuma hizo ni propaganda zisizo na ukweli wala msingi. Amesema makala hiyo iliyoashiria kuwa serikali ya Buhari imekuwa ikawaandama Wakristo na wapinzani tu wa kaskazini mwa nchi ni propaganda ambazo zinazipa nguvu harakati za kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram linalokwenda mbio kuwagawanya wananchi kwa misingi ya dini.

Kadhalika msemaji wa Rais Mohamadu Buhari wa Nigeria amelitaka gazeti hilo la London kuitembelea Nigeria na kufanya uchunguzi kuhusu madai hayo ya ubaguzi wa kidini badala ya kutegemea duru zisizo rasmi na za kipropaganda.

Hii ni katika hali ambayo, jopo la uchunguzi lililotwikwa jukumu la kuchunguza mauaji ya Waislamu kaskazini mwa Nigeria limekiri kuwa jeshi la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika liliuawa Waislamu zaidi ya 300 katika mji wa Zaria jimbo la Kaduna na kupendekeza kufunguliwa mashtaka wanajeshi waliouhusika na mauaji hayo ya kikatili mwishoni mwa mwaka jana 2015.