Askari wa Uganda wapandishwa kizimbani nchini Somalia
Duru za habari zimeripoti kuwa, askari kadhaa wa Uganda wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya kijeshi ya Uganda nchini Somalia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, askari 17 wanaohudumu katika kikosi cha askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM, walipandishwa kizimbani katika mahakama ya jeshi la Uganda iliyoko mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia. Askari hao wanatuhumiwa kwa kuuza zana za kijeshi na mafuta mjini Mogadishu.

Habari zaidi zinaripoti kuwa, katika kesi hiyo askari mmoja amepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela. Hii ni mara ya kwanza kuundwa mahakama ya kijeshi nchini Somalia kwa ajili ya kuwahukumu askari wanaohudumu katika kikosi cha askari wa kusimamia amani nchini humo AMISOM. Askari wa AU nchini Somalia wamekuwepo nchini humo kwa zaidi ya miaka tisa sasa.