Watu 148 wamefariki katika ajali ya boti nchini DRC
Idadi ya watu waliofariki dunia ilifikia 148 kutokana na ajali ya boti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mapema wiki hii.
Ajali hiyo ilitokea Jumanne jioni huko Mbandaka katika jimbo la Equateur.
Seneta Jean-Paul Boketsu Bofili wa jimbo la Equateur amesema kwamba watu 500 walikuwemo kwenye boti hiyo ya mbao yenye injini wakati ilipozama baada ya kushika moto.
Bofili amewaambia waandishi wa habari kwamba waliofariki dunia ni pamoja na watoto akiongeza kuwa mamia ya watu bado hawajulikani waliko, huku zaidi ya wahanga 150 wakiokolewa wakiwa na viwango tofauti vya kuungua kwa moto.
Amesema kuwa miili kadhaa iliyoungua imepatikana baada ya boti hiyo ya mbao kuteketea kwa moto.
Ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa boti ilishika moto wakati mwanamke mmoja alipokuwa akipika chakula ndani ya boti hiyo ya mbao.
Awali maafisa wa eneo hilo walikuwa wamesema kwamba watu waliofariki dunia ni 50 lakini kadiri siku zinavyopita, idadi hiyo imekuwa ikiongezeka na kufikia karibu 150.
Boti hiyo ya HB Kokolo ilikuwa inatumika kuunganisha abiria kutoka bandari ya Bolenge katika jimbo la Equateur kuelekea kwenye soko kuu la kijiji cha Ngbondo ambacho kinadhamini bidhaa za maeneo kadhaa.
Usafiri wa majini ndio usafiri Mkuu DRC kutokana na barabara kutopitika.
Ajali hiyo ilitokea siku chache baada ya zaidi ya watu 50 kupoteza maisha wakati mashua iliyokuwa imejaa mizigo ilipopinduka kwenye mto huo huo wa huko Mbandaka.