Umoja wa Mataifa: Unyanyasaji wa kingono na mauaji yaongezeka DRC
-
Wakimbizi DRC
Uchunguzi katika mikoa miwili ya mashariki mwa DRC ya Kivu Kaskazini na Kusini waonesha ukikwaji wa haki za binadamu umeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Tume maalum ya kuchunguza haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema raia wameripoti kuongezeka kwa matukio ya mauaji ya kinyume na sheria na unyanyasasi wa kingono mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa ya tume hiyo huru iliyofanya uchunguzi kwenye mikoa miwili ya mashariki mwa Kongo ya Kivu Kaskazini na Kusini ambayo imekumbwa na mripuko wa ugonjwa wa Ebola, imesema raia wamesimulia juu ya mgogoro mkubwa wa ukiukwaji haki za binadamu, unaotokana na madai ya unyanyasaji wa kingono na mauaji.
Taarifa hiyo imeeleza namna ambavyo hali ya usalama ilivyozorota na kusababisha wakaazi kuishi kwenye hatarai na kukosa ulinzi. Tume hiyo iliyoanzishwa na baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa imesema ilikutana na mashahidi na maafisa mjini Kinshasa na inatarajia kwenda Goma hali ya usalama itakapoimarika.
Ukatili wa kingono dhidi ya watoto limekuwa jambo la kawaida, la kimfumo na unazidi kuongezeka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Takwimu za nchi nzima zilizokusanywa na watoa huduma za ulinzi na jinsia zinaonyesha kuwa, katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka jana wa 2025, kulikuwa na zaidi ya kesi 35,000 za ukatili wa kingono dhidi ya watoto nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mwaka juzi wa 2024, watoto walikuwa wahanga wa karibu asilimia 40 ya matukio yote yaliyoripotiwa ya vitendo vya ukatili wa kingono; kiwango ambacho ni karibu mara tatu ya takwimu za mwaka 2020.
Migogoro ndio chanzo kikuu cha ukatili huu tajwa hata hivyo shirika la UNICEF limeripoti uwepo wa ukatili wa kingono dhidi ya watoto katika kila jimbo huko Kongo.