Baghaei: Iran inafuatilia hatua kwa hatua utekelezaji wa Marekani wa MoU
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139550-baghaei_iran_inafuatilia_hatua_kwa_hatua_utekelezaji_wa_marekani_wa_mou
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Tehran itafuatilia, dakika kwa dakika, iwapo Marekani itazingatia makubaliano ya maelewano (MoU) ya kumaliza vita, na akaonya kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitatekeleza wajibu wake chini ya makubaliano hayo ikiwa ni upande mmoja pekee unaoyatekeleza.
(last modified 2026-07-01T03:41:09+00:00 )
Jul 01, 2026 03:40 UTC
  • Esmail Baghaei
    Esmail Baghaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Tehran itafuatilia, dakika kwa dakika, iwapo Marekani itazingatia makubaliano ya maelewano (MoU) ya kumaliza vita, na akaonya kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitatekeleza wajibu wake chini ya makubaliano hayo ikiwa ni upande mmoja pekee unaoyatekeleza.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema:

"Kanuni ya 'utekelezaji wa wajibu kwa kubadilishana na utekelezaji wa wajibu' katika mazungumzo ina maana kwamba tutatekeleza wajibu wetu kwa muda ambao tu upande wa pili pia utakuwa unatekeleza wajibu wake."

Amesisitiza kuwa, "Hakuna wajibu wowote unaopaswa kutekelezwa na upande mmoja pekee."

Baghaei amesema hayo wakati Marekani na Iran bado zinatofautiana kuhusu utekelezaji wa waraka wa makubaliano (MoU) wenye vipengele 14, uliotiwa saini katikati ya mwezi Juni. Makubaliano hayo yalilenga kukomesha vita vya mashambulizi vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, pamoja na kuondoa mzingiro wa baharini uliowekwa dhidi ya Iran na kuachiliwa kwa mali za Iran zilizokuwa zimezuiwa nje ya nchi.

Baghaei amesema kuwa Tehran haikuwahi kutarajia mchakato wa kidiplomasia ungeendelea bila changamoto, kutokana na kutokuaminiana kwa kiwango kikubwa kati ya pande hizo mbili, pamoja na uzoefu mchungu wa Iran kuhusu Marekani kuvunja ahadi zake mara kwa mara na utawala wa Kizayuni kuhujumu juhudi za kidiplomasia.