Kanisa Katoliki Tanzania laitaka serikali kumuachilia huru Tundu Lissu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125410-kanisa_katoliki_tanzania_laitaka_serikali_kumuachilia_huru_tundu_lissu
Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki nchini Tanzania (TEC) limetoa wito kwa serikali kuwaachilia bila masharti viongozi wa kisiasa waliokamatwa kwa kudai haki, likisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda amani ya taifa, hasa kuelekea mwaka wa uchaguzi.
(last modified 2025-04-20T08:38:35+00:00 )
Apr 20, 2025 08:38 UTC
  • Kanisa Katoliki Tanzania laitaka serikali kumuachilia huru Tundu Lissu

Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki nchini Tanzania (TEC) limetoa wito kwa serikali kuwaachilia bila masharti viongozi wa kisiasa waliokamatwa kwa kudai haki, likisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda amani ya taifa, hasa kuelekea mwaka wa uchaguzi.

Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa, amesema kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa kutumia nguvu bali kwa maridhiano na haki, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani ya nchi kwa kuhakikisha mifumo ya uchaguzi inarekebishwa ili kutoa nafasi kwa upatikanaji wa viongozi wa haki na wa kweli.

Kauli ya Askofu Pisa imekuja wakati ambapo mjadala wa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na ushiriki wa vyama vya siasa umekuwa ukitawala anga ya kisiasa nchini, huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu kukamatwa kwa viongozi wao wakubwa akiwamo Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Tundu Lissu Tundu Lissu, na ukosefu wa haki katika uendeshaji wa siasa.

Akizungumza katika mkesha wa Pasaka uliofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Andrea Kagwa, Jimbo Katoliki Lindi, Askofu huyo amesema kuwa kama kurudi mezani ndiko kunakoweza kulinda amani, basi kila anayehamasisha hilo anapaswa kuungwa mkono, si kukandamizwa au kukamatwa.

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA kimevitaka vyombo vya dola vimruhusu Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Tundu Lissu kuonana na mawakili na jamaa zake.