UN: Operesheni za misaada na mapigano Kaskazini mwa Darfur, Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125454-un_operesheni_za_misaada_na_mapigano_kaskazini_mwa_darfur_sudan
Mashirika ya misaada yanakumbana na matatizo makubwa katika kukabiliana janga la kibinadamu linalozidi kuwa baya Kaskazini mwa Darfur, Sudan, linalosababishwa na mashambulizi ya waasi wa kundi la Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
(last modified 2025-04-21T07:06:32+00:00 )
Apr 21, 2025 07:06 UTC
  • UN: Operesheni za misaada na mapigano Kaskazini mwa Darfur, Sudan

Mashirika ya misaada yanakumbana na matatizo makubwa katika kukabiliana janga la kibinadamu linalozidi kuwa baya Kaskazini mwa Darfur, Sudan, linalosababishwa na mashambulizi ya waasi wa kundi la Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Clementine Nkweta-Salami, amesema katika taarifa iliyotolewa usiku wa Jumapili kwamba upatikanaji wa misaada ya kibinadamu umeendelea kuwa “hatari kupita kiasi” katika mji mkuu wa Darfur Kaskazini, wa el-Fasher na maeneo yanayouzunguka, ambako RSF imetekeleza mashambulizi kadhaa katika wiki za hivi karibuni.

Mashambulizi hayo yamesababisha watu wengi kukimbia kutoka katika kambi za wakimbizi za Zamzam, Abu Shouk na nyinginezo – hali ambayo ni “ya kubadilika kila mara” na “isiyotabirika,” huku kukiwa na hofu kwamba RSF inajiandaa kwa mashambulizi makubwa zaidi.

Miaka miwili tangu kuanza kwa mgogoro wake na serikali ya Sudan, waasi wa RSF wameshambulia kambi za Zamzam – inayosemekana kuwa na hadi watu milioni moja – na Abu Shouk zaidi ya wiki moja iliyopita, na kuua angalau watu 300 na kuwalazimisha hadi watu 400,000 kukimbia umbali wa kilomita 60 kupitia jangwa hadi mji wa Tawila.

Katika taarifa yake, Nkweta-Salami amesema kuwa hadi watu 450,000 waliokoseshwa makazi wanazidi “kukatwa kutoka kwa minyororo ya usambazaji na msaada,” jambo linalowaweka katika hatari kubwa ya milipuko ya magonjwa, utapiamlo na njaa.

Ametoa wito kwa mashirika ya UN na mashirika yasiyo ya kiserikali kuruhusiwa “kupata fursa ya haraka na endelevu ya kuingia maeneo haya ili kuhakikisha msaada wa kuokoa maisha unaweza kutolewa kwa usalama na kwa kiwango kikubwa.”

Mgogoro huo umegawanya Sudan katika pande mbili, jeshi likidhibiti kaskazini na mashariki, huku waasi wa RSF wakidhibiti sehemu kubwa ya Darfur na maeneo ya kusini. Serikali ya Sudan inasema Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ni muungaji mkono wa waasi wa RSF ambao imesema wanatekeleza mauaji ya kimbari.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu, kuwahamisha zaidi ya watu milioni 15, na kuunda kile ambacho UN imekielezea kama janga baya zaidi la kibinadamu duniani.