Waasi wa RSF wameua raia 300 huko Al-Nahud
Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Sudan imetangaza kwamba raia wasiopungua 300, wakiwemo watoto 21 na wanawake 15, wameuawa katika shambulio lililofanywa na waasi wa RSF katika mji wa Al-Nahud, jimbo la Kordofan Magharibi.
Katika taarifa rasmi, tume hiyo imelaani “ukiukaji uliofanywa na waasi wa RSF dhidi ya raia huko Al-Nahud, ikiwa ni pamoja na kuwalenga moja kwa moja raia na kuwaua kiholela.”
Taarifa hiyo imesema kwamba idadi ya vifo iliyotolewa bado ni ya awali kutokana na mji huo kuendelea kuzingirwa na wapiganaji wa RSF, ambao wamezuia wakazi kukimbia au kupata misaada.
Ijumaa iliyopita, Mtandao wa Madaktari wa Sudan uliripoti vifo zaidi ya 100 katika shambulio hilo. Kwa mujibu wa tume hiyo, RSF pia ilipora vifaa vya matibabu, masoko ya eneo hilo na Hospitali ya Al-Nahud.
RSF ilidai Ijumaa kwamba imechukua udhibiti kamili wa Al-Nahud na kushika makao makuu ya Kikosi cha 18 cha askari wa jeshi la Sudan baada ya mapigano na jeshi hilo la serikali.
Mji huo, ambao awali ulikuwa chini ya udhibiti wa jeshi la taifa, ulikuwa ukitumika kama mji mkuu wa muda wa Kordofan Magharibi tangu Julai 2024, baada ya RSF kushika mji mkuu wa awali, Al-Fula.
Tangu Aprili 15, 2023, RSF imekuwa ikipigana na jeshi kwa udhibiti wa Sudan, hali ambayo imesababisha maelfu ya vifo na kuibua moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya Wasudani 20,000 wameuawa na wengine milioni 15 wamelazimika kuhama tangu vita vianze. Serikali ya Sudan inatuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuunga mkono kundi la waasi wa RSF linalotekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari nchini humo.