Misri: Haiwezekani kupuuza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Israel
-
Jasmine Moussa
Mwakilishi wa Misri katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) amesema: "Katika muda mrefu, haiwezekani kupuuza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, kama chombo kikuu cha mahakama cha Umoja wa Mataifa."
Jasmine Moussa amesema kuwa, Misri inaunga mkono suala la Palestina katika nyanja zote za kisiasa na kisheria, na kwamba msimamo wa nchi hiyo katika suala hilo uko wazi na thabiti.
Ameongeza kuwa: "Mashtaka yaliyowasilishwa kuhusiana na kadhia ya Palestina hususan kwa kuzingatia hali mbaya ya maafa katika Ukanda wa Gaza, yameunda kipindi muhimu sana kwa mapambano ya Palestina."
Mwakilishi wa Misri katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu amesisitiza kuwa: "Kile Israel inachofanya katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ni kitendo ambacho kinakiuka sheria za kimataifa, na walimwengu wanasubiri kutolewa hukumu ya ICC katika miezi ijayo ili harakati pana za kisiasa zianze katika ngazi ya taasisi za Umoja wa Mataifa."
Jasmine Moussa amesema: "Wawakilishi wa nchi nyingi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai wametangaza uungaji mkono wao kamili kwa haki za watu wa Palestina, ikiwemo haki ya kujitawala." Amesema nchi zipatazo 40 pia zimesisitiza haja ya Israel kutekeleza wajibu wake kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa, hususan kuhusu shughuli za mashirika ya kimataifa katika ardhi za Palestina, kuondoa mzingiro wa Gaza, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inaingia katika eneo hilo.