Machafuko yazidi katika kambi ya Zamzam iliyozingirwa katika eneo la Darfur, Sudan
(last modified Mon, 05 May 2025 06:27:12 GMT )
May 05, 2025 06:27 UTC
  • Machafuko yazidi katika kambi ya Zamzam iliyozingirwa katika eneo la Darfur, Sudan

Mgogoro nchini Sudan uliolipuka miaka miwili iliyopita umechochea wimbi la vurugu za kikabila, kuunda janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani, na kuingiza maeneo kadhaa ya nchi katika njaa.

Mwezi Aprili, mapigano kati ya jeshi la Sudan na waasi wa RPF yaliingia kwenye moja ya makambi makubwa ya watu waliokoseshwa makazi kutokana na vita vya miaka mingi: kambi kubwa ya Zamzam katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan, makazi ya takriban watu nusu milioni.

Mashahidi walielezea tukio la wanajeshi wa RSF kuvamia kambi ya Zamzam tarehe 11 Aprili, wakipora na kuchoma nyumba huku makombora yakishuka na ndege zisizo na rubani zikiruka juu.

RSF waliteka kambi hiyo kubwa mwezi Aprili baada ya siku kadhaa za mashambulizi ya makombora, ndege zisizo na rubani na mashambulizi ya ardhini ambayo Umoja wa Mataifa unasema yaliua angalau watu 300 na kulazimisha takriban watu 400,000 kukimbia — moja ya ukiukaji mbaya zaidi tangu vita kuanza.

Hayo yanajiri wakati ambao Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imevituhumu Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwa kufanya "mauaji ya halaiki" dhidi ya raia huko Al-Nahud katika jimbo la Kordofan Magharibi, kusini mwa nchi na kusababisha vifo vya watu 300.

RSF ilikuwa haijatoa taarifa yoyote kuhusu tuhuma hizo lakini kundi hilo lilitangaza kuwa limechukua udhibiti wa El-Khuwei huko Kordofan Magharibi, siku moja baada ya kuiteka Al-Nahud kusini mwa Sudan.

Tangu Aprili 15, 2023, RSF imekuwa ikipigana na jeshi kwa udhibiti wa Sudan, hali ambayo imesababisha maelfu ya vifo na kuibua moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya Wasudani 20,000 wameuawa na wengine milioni 15 wamelazimika kuhama tangu vita vianze. Serikali ya Sudan inatuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuunga mkono kundi la waasi wa RSF linalotekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari nchini humo.