UN: Maafisa usalama Sudan Kusini wameua na kubaka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12613-un_maafisa_usalama_sudan_kusini_wameua_na_kubaka
Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Sudan Kusini kuwachukulia hatua za kisheria maafisa usalama walioua raia na kunajisi wanawake na mabinti wadogo katika machafuko ya mwezi uliopita katika mji mkuu Juba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 04, 2016 10:37 UTC
  • UN: Maafisa usalama Sudan Kusini wameua na kubaka

Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Sudan Kusini kuwachukulia hatua za kisheria maafisa usalama walioua raia na kunajisi wanawake na mabinti wadogo katika machafuko ya mwezi uliopita katika mji mkuu Juba.

Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema raia zaidi ya 73 wameuawa katika mapigano hayo ya Juba hadi sasa na yumkini idadi hiyo ikawa kubwa zaidi. Aidha amesema umoja huo umerekodi kesi 217 za ubakaji kati ya Julai 8-25 wakati yaliposhtadi mapigano hayo kati ya askari wanaomuunga mkono Rais Salva Kiir na wanajeshi waitifaki wa Makamu wa Kwanza wa Rais aliyeutoroka mji wa Juba, Riek Machar ambaye wadhifa wake kwa sasa unashikiliwa na Taban Deng Gai, aliyekuwa waziri wa upande wa upinzani.

Wanajeshi wa Sudan Kusini

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za dharura ili kukomesha mapigano hayo ya Juba na mgogoro wa kisiasa nchini humo kwa ujumla.

Salva Kiir na Riek Machar wakisaini makubaliano ya amani Agosti 2015

Machafuko mapya mjini Juba yamepelekea kuuawa watu wasiopungua 300 hadi sasa wengi wao wakiwa maafisa usalama. Aidha makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kuitoroka nchi na kuwa wakimbizi katika nchi jirani na haswa Uganda.