Jiji la Port Sudan lashambuliwa kwa ndege isiyo na rubani kwa siku ya tano mfululizo
(last modified Thu, 08 May 2025 10:44:56 GMT )
May 08, 2025 10:44 UTC
  • Jiji la Port Sudan lashambuliwa kwa ndege isiyo na rubani kwa siku ya tano mfululizo

Jiji la Port Sudan, mashariki mwa Sudan, Alhamisi asubuhi limekumbwa na shambulio jipya la ndege isiyo na rubani (drone) kwa siku ya tano mfululizo, huku mapigano makali yakiendelea kati ya jeshi na waasi wa RSF.

Kwa mujibu wa mashuhuda, milipuko ilisikika jijini humo ambapo kikosi cha ulinzi wa anga cha  jeshi la Sudan kilijibu shambulio hilo lililodumu kwa takriban dakika 45. Mashuhuda hao wamesema shambulio hilo la droni lililenga makao makuu ya chuo cha jeshi la anga kilichopo Port Sudan.

Jiji hilo lililoko katika ufukwe wa Bahari Nyekundu limekuwa makao ya muda ya  serikali ya Sudan kufuatia kuzuka kwa mapigano na RSF tangu Aprili 2023.

Maafisa wa Sudan mara kadhaa wameilaumu RSF kwa kufanya mashambulio ya ndege zisizo na rubani dhidi ya miundombinu ya kiraia, vikiwemo vituo vya umeme na maeneo mengine muhimu, katika miji ya kaskazini kama Merowe, Dongola, Dabba na Atbara.

Tangu Aprili 2023, RSF imekuwa ikipambana na jeshi kwa ajili ya kudhibiti Sudan, hali iliyosababisha maelfu ya vifo na kuibua moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Serikali ya Sudan ilitangaza Jumanne kwamba imeamua kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kumrejesha nyumbani balozi wake, ikitangaza kuwa Imarati ni "nchi chokozi."

Yassin Ibrahim Yassin, Waziri wa Ulinzi wa Sudan, amesema hayo kupitia televisheni ya serikali ambapo ameishutumu Abu Dhabi kwa kutoheshimu haki ya kujitawala ardhi ya Sudan kupitia kushirikiana kwake na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vinavyopigana na Jeshi la Sudan SAF kwa muda mrefu sasa. 

Amesema uamuzi huo umechochewa na msaada wa kijeshi unaotolewa na Imarati kwa RSF, ikiwa ni pamoja na kuwapa silaha za kisasa zilizotumika katika mashambulizi ya hivi karibuni ya droni na ndege zisizo na rubani pamoja na makombora, kupiga bandari, uwanja wa ndege na vituo vya umeme vya mji wa Port Sudan.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za ndani, watu zaidi ya 20,000 wameuawa na milioni 15 wamepoteza makazi. Hata hivyo, utafiti wa wataalamu wa Marekani unaeleza kuwa idadi ya vifo huenda imefikia takriban 130,000.