Somalia yasajili wapiga kura baada ya miaka 56 ya kutokuwa na upigaji kura
Zaidi ya miaka 56 tangu raia wa Somalia katika upigaji kura wa moja kwa moja, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka ya Somalia imeanzisha mchakato mkubwa wa kusajili wapiga kura.
Ni wachache tu nchini humo ambao wamewahi kupiga kura katika maisha yao, ikiwa ni pamoja na Rais Hassan Sheikh Mohamud, ambaye alikuwa na miaka 15 mwaka 1969 wakati Somalia ilipoendesha uchaguzi wa haki ya kupiga kura moja kwa moja.
Hamasa ya kushiriki katika uchaguzi wa bunge na urais unaopangwa kufanyika Mei 2026 imepelekea foleni ndefu mjini Mogadishu, ambapo wananchi wamepuuza vitisho vya kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab na kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kama wapiga kura.
Tofauti na miaka ya hivi karibuni, ambapo wazee wa koo na wawakilishi waliowachagua wabunge walikuwa wakificha utambulisho kwa kufunika nyuso zao kwa hofu ya Al-Shabaab, sasa wananchi wanajitokeza kwa wingi na kwa ujasiri kujitokeza ili kujisajili katika daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa mabaraza ya mitaa na uchaguzi wa kitaifa kuchagua wabunge, maseneta, na rais.
Katika uchaguzi wa 2022, wazee wa koo na wawakilishi — ambao wanakadiriwa kuwa 14,200 — walichagua wabunge 328 na maseneta, ambao walimchagua rais.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka (NIEBC) Abdikarim Ahmed Hassan, na timu yake ya wanachama 17 walizindua mchakato wa usajili mjini Mogadishu hivi karibuni , ambao unatarajiwa kuendelea hadi Mei 15, 2025.
Hassan amesema: “Tutaendelea kwenda katika majimbo mengine ya shirikisho, kuanzia na South West, Jubbaland, Puntland na sehemu zote za Somalia."
Somalia ina majimbo sita ya shirikisho: Puntland, Jubbaland, South West, Hirshabelle, Galmudug, na Somaliland.
Mwenyekiti huyo amesemakwamba katika nchi ambapo taasisi za sSerikali zilivunjika kabisa baada ya Rais Siad Barre kuondolewa madarakani mwaka 1991, zaidi ya asilimia 90 ya watu hawajawahi kupiga kura kwa viongozi wao.
Tume inakusudia kusajili wapiga kura milioni nne nchini kote, huku milioni 1.5 wakitarajiwa kutoka Mogadishu pekee.
Wale watakaosajiliwa watatumia haki yao ya kupiga kura mwezi Juni mwaka huu, wakati Mogadishu itakapofanya uchaguzi wake wa kwanza wa mabaraza tangu 1969, kisha kufuatiwa na uchaguzi wa wabunge na rais Mei 2026, pamoja na kura ya maoni kutunga katiba ya mpito.