Amnesty International yaikosoa Rwanda kuwakubali waliofurushwa kutoka Marekani
(last modified Wed, 14 May 2025 11:18:56 GMT )
May 14, 2025 11:18 UTC
  • Amnesty International yaikosoa Rwanda kuwakubali waliofurushwa kutoka Marekani

Uamuzi wa Rwanda wa kuwakubali waliofurushwa kutoka Marekani umekosolewa na Amnesty International, shirika hili likidai kuwa makubaliano hayo yanakiuka yanakiuka mkataba wa wakimbizi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kupitia kwa mwanaharakati wake mkuu Christian Rumu pia limekosoa mchakato wa kupata hifadhi kwa wahamiaji hao kwamba pia una hatari ya kukiuka sheria ya kimataifa ya uhamiaji na kwamba bado hakuna uhakika kuhusu mafanikio yake.

Amnesty International imechukulia mfano wa makubaliano kati ya Rwanda na Uingereza mwaka 2022, wa kuwapa hifadhi maelfu ya wakimbizi, kabla ya Waziri Mkuu wa Uingereza aliyechaguliwa Keir Starmer kubatilisha.

Alipoingia madarakani, Rais wa Marekani Donald Trump, alianzisha sheria kali punde baada ya kuapishwa kwa muhula wa pili wa kuwafurisha raia wote wa kigeni walio nchini humo bila ya kuwa na vibali vya kuishi.

Rwanda ilisema ina uwezo wa kusaidia kupunguza mateso ya nchi nyingi za Ulaya na Marekani, hata hivyo watetezi wa haki za binadamu kwa muda mrefu wameelezea wasiwasi wao kuhusu vifo vya watu wanaoshukiwa kuwa wakosoaji wa serikali nchini Rwanda, pamoja na madai ya mauaji ya watu wengine ambao wametafuta uhamisho katika nchi kama vile Afrika Kusini.