Al-Qaeda yatangaza kuhusika na mashambulizi ya Burkina Faso, yasema imeua wanajeshi 60
(last modified Thu, 15 May 2025 10:56:15 GMT )
May 15, 2025 10:56 UTC
  • Al-Qaeda yatangaza kuhusika na mashambulizi ya Burkina Faso, yasema imeua wanajeshi 60

Kundi lenye mafungamano na al-Qaeda, JNIM, limetangaza kuhusika na shambulio lililofanyika katika eneo la kijeshi kwenye jimbo la Loroum kaskazini mwa Burkina Faso, likidai kuwaua wanajeshi 60.

Shirika la kiintelijensia la Marekani, SITE ambalo hufuatilia harakati za makundi ya kigaidi mtandaoni, limesema kundi hilo lilichapisha jumbe siku za Jumatatu na Jumanne ikidai kuhusika na mashambulizi manne nchini Burkina Faso na Mali.

Mashambulizi haya yanaangazia changamoto kubwa za kiusalama zinazozikabili nchi tatu za Sahel (Burkina Faso, Mali na Niger) katika kukabiliana na uasi na mashambulizi yanayoongezeka.

Mamlaka nchini Burkina Faso bado haijatoa maoni yoyote rasmi kuhusu mashambulizi yaliyotokea nchini humo wiki hii.

Kwa mujibu wa SITE, mashambulizi makubwa zaidi yalitokea katika mji wa Sourou, ambapo wapiganaji wa JNIM walivamia eneo la jeshi na kuua makumi ya wanajeshi. Shirika hilo halikutaja tarehe ya shambulio hilo.

Awali shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) liliripoti kuwa kundi lenye silaha lililenga vijiji vinavyoaminika kulisaidia jeshi la taifa, na kuua takriban raia 100 karibu na eneo la Solenzo nchini Burkina Faso.